• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Dortmund wapoteza mechi ya Bundesliga licha ya Haaland kuwafungia mabao matatu

Dortmund wapoteza mechi ya Bundesliga licha ya Haaland kuwafungia mabao matatu

Na MASHIRIKA

BORUSSIA Dortmund walipokezwa kichapo cha 4-3 kutoka kwa Bochum licha ya Erling Braut Haaland kuwafungia mabao matatu katika mchuano wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) uliowakutanisha ugani Signal Iduna Park mnamo Jumamosi.

Wenyeji Dortmund walijipata chini kwa mabao 2-0 kufikia dakika ya nane kabla ya Haaland kupachika wavuni mabao mawili kupitia penalti na kuongeza la tatu katika dakika ya 62.

Hata hivyo, Bochum waliofunga magoli yao kupitia kwa Sebastian Polter na Gerrit Holtmann walirejea mchezoni na kuzamisha chombo cha Dortmund mwishoni mwa kipindi cha pili.

Jurgen Locadia alisawazishia Bochum katika dakika ya 81 kabla ya Milos Pantovic kufunga penalti ya ushindi dakika nne baadaye.

Dortmund wanasalia katika nafasi ya pili kwa alama 63 huku pengo la pointi 12 likitamalaki kati yao na Bayern Munich ambao tayari wametawazwa mabingwa wa Bundesliga zikisalia mechi mbili pekee kabla ya kampeni za msimu huu kutamatika rasmi.

Bayer Leverkusen wanakamata nafasi ya tatu kwa alama 55 sawa na SC Freiburg wanaofunga orodha ya nne-bora.

Haaland, 21, sasa amefungia Dortmund mabao 21 kutokana na mechi 22 za Bundesliga msimu huu. Ana jumla ya mabao 28 kutokana na mechi 28 za mashindano yote.

MATOKEO YA BUNDESLIGA (Jumamosi):

Mainz 3-1 Bayern Munich

Dortmund 3-4 Bochum

Arminia 1-1 Hertha Berlin

Augsburg 1-4 Cologne

Stuttgart 1-1 Wolfsburg

Hoffenheim 3-4 Freiburg

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Mainz yaduwaza Bayern Munich katika Bundesliga

Ancelotti aweka historia ya kushinda mataji ya ligi katika...

T L