• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Argentina pua na mdomo kufuzu kwa Kombe la Dunia baada ya kukung’uta Uruguay

Argentina pua na mdomo kufuzu kwa Kombe la Dunia baada ya kukung’uta Uruguay

Na MASHIRIKA

ARGENTINA wanatarajiwa kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia nchini Qatar baada ya kusajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Uruguay.

Angel Di Maria alifunga bao la pekee na la ushindi katika mchuano huo. Argentina almaarufu La Albiceleste, sasa wanashikilia nafasi ya pili kwenye kundi la vikosi 10 vya Amerika Kusini. Masogora hao wa kocha Lionel Scaloni wamejizolea alama 28, sita nyuma ya viongozi Brazil watakaovaana nao mnamo Novemba 16, 2021.

Brazil ambao ni mabingwa mara tano wa Kombe la Dunia tayari wamejikatia tiketi ya kuelekea Qatar baada ya kupepeta Colombia 1-0 mnamo Novemba 12, 2021. Uruguay ambao wamepoteza mechi tatu zilizopita mfululizo, wanashikilia nafasi ya sita kwa alama 16 sawa na Colombia na Chile wanaofunga orodha ya nne bora watakaofuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia.

Ushindi kwa Argentina dhidi ya Brazil utawakatia tiketi ya kunogesha fainali zijazo za Kombe la Dunia iwapo Uruguay, Colombia na Chile watapoteza mechi zao. Uruguay walipoteza nafasi nyingi za wazi na utepetevu wao ukaruhusu Di Maria kuwafunga baada ya kushirikiana vilivyo na Paulo Dybala.

Lionel Messi aliletwa ugani katika dakika 15 za mwisho licha ya kwamba bado hakuwa katika hali shwari ya kuwajibishwa. Nyota huyo bado hajafungia waajiri wake Paris Saint-Germain (PSG) bao lolote ligini tangu abanduke Barcelona na kujiunga nao mwanzoni mwa msimu huu wa 2021-22.

Katika mchuano mwingine, Peru walikomoa Bolivia 3-0 mjini Lima na kupaa hadi nafasi ya saba kwa alama 14, mbili kuliko Paraguay na Bolivia. Venezuela wanavuta mkia kwa alama saba baada ya kushinda mechi mbili, kuambulia sare mara moja na kupoteza mechi 10 kati ya 13 za hadi kufikia sasa.

You can share this post!

Serikali yahimizwa kubuni wizara ya masuala na mikakati ya...

Ramsey apachika wavuni mabao mawili na kusaidia Wales...

T L