• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
Atletico Madrid yakatiza safari ya Man-United kwenye soka ya UEFA msimu huu

Atletico Madrid yakatiza safari ya Man-United kwenye soka ya UEFA msimu huu

Na MASHIRIKA

KAMPENI ya Manchester United katika soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu ilifika ukingoni mnamo Jumanne baada ya miamba hao wa Uingereza kudenguliwa na Atletico Madrid kwa jumla ya mabao 2-1.

Chini ya kocha mshikilizi Ralf Rangnick, Man-United walipokezwa na Atletico ya Uhispania kichapo cha 1-0 katika mchuano wa mkondo wa pili Jumanne usiku ugani Old Trafford.

Renan Lodi alicheka na nyavu za Man-United katika dakika ya 41 na hivyo kusaidia waajiri wake waliolazimishiwa sare ya 1-1 katika mkondo wa kwanza nchini Uhispania kufuzu kwa hatua ya robo-fainali.

Ingawa Man-United walitamalaki mchezo na kuonekana kuwazidi wageni wao maarifa katika takriban kila idara, Atletico walibana sana ngome yao huku kipa Jan Oblak akijituma maradufu kupangua makombora kutoka kwa wavamizi wa Man-United.

Kudenguliwa kwa Man-United kwenye hatua ya 16-bora ya UEFA sasa kunazima matumaini yao ya kujinyanyulia taji lolote msimu huu na hivyo kuendeleza ukame wa miaka mitano bila kombe lolote kabatini mwao.

Kufikia sasa, Man-United wanashikilia nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 50, moja nyuma ya Arsenal ambao wana mechi tatu zaidi za kutandaza ili kufikisha idadi ya michuano 29 ambayo imesakatwa na Man-United.

Sawa na Atletico waliopepeta Cadiz 2-1 katika mchuano wao wa awali katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Man-United nao walikuwa na ari ya kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 3-2 dhidi ya Tottenham Hotspur katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Machi 12, 2022.

Ushindi huo wa Man-United uliweka hai matumaini yao finyu ya kukamilisha kampeni za EPL msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora na hivyo kufuzu kwa soka ya UEFA muhula ujao wa 2022-23.

Man-United walikamilisha kampeni zao za makundi kwenye UEFA msimu huu kileleni mwa Kundi F baada ya kujizolea alama 11 kutokana na mechi sita. Mabingwa hao mara 20 wa EPL walibandua Paris Saint-Germain (PSG) katika hatua ya 16-bora ya UEFA mnamo 2018-19 kwa kanuni ya bao la ugenini.

Walitoka chini baada ya kichapo cha 2-0 katika mkondo wa kwanza nchini Ufaransa na kupepeta PSG 3-1 katika marudiano ugani Old Trafford. Hata hivyo, walishindwa kusonga mbele zaidi ya hatua ya makundi mnamo 2020-21 na hatimaye wakashuka hadi Europa League ambapo walizidiwa ujanja na Villarreal ya Uhispania.

Chini ya mkufunzi Diego Simeone, Atletico sasa wameshinda mechi nne zilizopita za La Liga na wanakamata nafasi ya nne jedwalini kwa pointi 51 sawa na Barcelona. Kivumbi cha UEFA ndilo pambano la pekee ambalo sasa linawapa Atletico matumaini finyu ya kujizolea taji msimu huu.

Mabingwa hao watetezi wa La Liga walikamilisha kampeni zao za Kundi B kwenye UEFA kwa alama saba, 11 nyuma ya Liverpool ambao tayari wametinga robo-fainali baada ya kubandua Inter Milan ya Italia kwa mabao 2-1.

Ingawa Atletico walidenguliwa na Chelsea kwenye hatua ya 16-bora ya UEFA msimu jana, kikosi hicho kimetinga robo-fainali za kipute hicho mara sita chini ya misimu minane iliyopita chini ya Simeone. Aidha, wanajivunia rekodi ya kushinda mechi 10 kati ya 13 dhidi ya mpinzani anayeshiriki soka ya EPL katika hatua za muondoano za UEFA.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Sossion aahidi kushirikiana na wafanyabiashara

Benfica yakomoa Ajax na kuingia robo-fainali za UEFA

T L