• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Barabara zote zaelekea Nyayo warembo wa Harambee Starlets wakivaana na Indomitable Lionesses

Barabara zote zaelekea Nyayo warembo wa Harambee Starlets wakivaana na Indomitable Lionesses

NA TOTO AREGE

TIMU ya taifa ya Kenya ya wanawake Harambee Starlets leo Jumanne, inashuka dimbani dhidi ya Indomitable Lionesses ya Cameroon katika mechi ya mkondo wa pili kufuzu Kombe la Wanawake la Mataifa ya Afrika (WAFCON) 2024, katika uwanja wa Nyayo kuanzia saa tisa jioni.

Starlets chini ya kocha Beldine Odemba, walipigwa 1-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyochezwa Ijumaa, Septemba 22, 2023, mjini Douala, Cameroon.

Bao hilo la pekee lilifungwa na mshambulizi Eliane Mambalamo dakika za mwanzo kipindi cha kwanza.

Mechi hiyo ilipigwa ugani Stade De Reunification de Douala nchini Camaeroon.

Sasa Kenya ina kibarua kikubwa leo Jumanne kwani ni lazima ipige Cameroon kwa tofauti ya mabao mawili au ushindi wa 1-0 ili kuenda moja kwa moja kwa penalti.

“Wasichana wamekuwa wakijituma kambini katika mazoezi. Hata baada ya kupoteza mechi dhidi ya Cameroon bado tuna nafasi ya kufuzu WAFCON. Tuko tayari kupigana tena,” alisema Odemba.

Alipoulizwa kuhusiana na kupoteza mechi yao dhidi ya Cameroon, Odemba alieleza kuwa: “Tulicheza kulingana na mpango wetu wa mchezo lakini wakati mwingine uoga wa kucheza ugenini, mchezaji wa 13 uwanjani na kuwa Starlets walikuwa hawajacheza kwa muda mrefu kwenye jukwaa kubwa, iliwachukua wasichana muda mrefu kurejea mchezoni.”

Mara ya mwisho timu hizo mbili zilikutana katika mechi ya kufuzu mchujo ya kufuzu WAFCON mnamo 2006. Kenya ilipoteza kwa jumla ya mabao 9-0. Starlets ilipoteza 5-0 nyumbani na 4-0 ugenini.

Mshindi wa jumla atakutana na mshindi kati ya Gabon na Botswana. Ijumaa wiki jana, Botswana iliifunga Gabon 4-1 ugenini na kuweka matumaini ya kufuzu mashindano hayo.

Nae nahodha Ruth Ingotsi aliwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuwashabikia.

“ Kwa sababu tutakuwa nyumbani, tunahitaji uwepo wao uwanjani. Tuna ahidi tutawapa matokeo mazuri kwa sababu bado tuna nafasi kubwa ya kufuzi,” alisema Ingotsi.

  • Tags

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Ongezeko la taka za kielektroniki tishio kwa...

Waathiriwa wa moto katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Hazina...

T L