• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Barcelona yakomoa Levante na kuingia nafasi ya pili La Liga

Barcelona yakomoa Levante na kuingia nafasi ya pili La Liga

Na MASHIRIKA

BARCELONA waliendeleza makali yao katika kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu kwa kutoka nyuma na kuzamisha chombo cha Levante 3-2 licha ya wenyeji wao hao kupokezwa penalti tatu katika kipindi cha pili.

Levante waliwekwa kifua mbele kupitia penalti ya Jose Luis Morales katika dakika ya 52 baada ya beki Son kuchezewa visivyo na Dani Alves. Dakika nne baadaye, Levante walipewa penalti ya pili baada ya Eric Garcia kunawa mpira ndani ya kijisanduku. Hata hivyo, mkwaju huo uliochanjwa na Roger ulipanguliwa na kipa wa Barcelona, Marc-Andre ter Stegen.

Barcelona walijibu mapigo hayo ya Levante kupitia bao la Pierre-Emerick Aubameyang aliyejaza kimiani krosi ya Ousmane Dembele. Ujio wa Gavi ulibadilisha kasi ya mchezo katika safu ya mbele ya Barcelona na chipukizi huyo akachangia bao la pili lililofumwa wavuni na Pedri Gonzalez.

Maxi Gomez alikabiliwa visivyo na Clement Lenglet ndani ya kijisanduku na tukio hilo likachangia penalti nyingine ambayo Levante walifungiwa na Gonzalo Melero katika dakika ya 83. Ingawa bao hilo liliwarejesha wenyeji mchezoni, Luuk de Jong alikamilisha krosi ya kichwa kutoka kwa Jordi Alba na Barcelona wakaondoka ugenini na alama tatu muhimu.

Barcelona sasa wameshinda mechi 11 na kuambulia sare mara nne kutokana na mechi 15 zilizopita katika La Liga. Chini ya kocha Xavi Hernandez, kikosi hicho kwa sasa kinashikilia nafasi ya pili jedwalini kwa alama 60 sawa na nambari mbili Sevilla ambao wametandaza mechi moja zaidi. Real Madrid wanaselelea kileleni mwa alama 12 zaidi huku zikisalia mechi saba pekee kwa kipute cha La Liga muhula huu kutamatika rasmi.

MATOKEO YA LA LIGA (Jumapili):

Levante 2-3 Barcelona

Osasuna 1-0 Alaves

Espanyol 1-0 Celta Vigo

Elche 1-2 Real Sociedad

You can share this post!

Wafanyakazi wa kampuni ya KPLC washtakiwa kwa wizi

Mkenya Ouna namba nne bora nchini Rwanda

T L