• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 9:35 AM
Brazil wakung’uta Ecuador 2-0 katika mechi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2022

Brazil wakung’uta Ecuador 2-0 katika mechi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2022

Na MASHIRIKA

FOWADI Richarlson Andrade wa Everton alifunga bao na kusaidia timu ya taifa ya Brazil kupepeta Ecuador 2-0 mnamo Ijumaa usiku katika mechi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Ushindi huo wa Brazil uliwadumisha kileleni mwa jedwali la vikosi vinavyowania kufuzu kwa fainali hizo za Kombe la Dunia kutoka Amerika Kusini.

Neymar Jr wa Paris Saint-Germain (PSG) alifunga bao la pili la Brazil kupitia penalti iliyotokana na tukio la fowadi Gabriel Jesus wa Manchester City kuchezewa visivyo ndani ya kijisanduku.

Brazil kwa sasa wameshinda mechi zote tano za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 na wanadhibiti kilele cha vikosi 10 kutoka Amerika Kusini kwa alama 15, nne zaidi kuliko nambari mbili Argentina.

Ecuador wanashikilia nafasi ya tatu kwa pointi tisa baada ya kushinda mechi tatu kati ya nne za kufuzu. Licha ya kutamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira, Brazil walifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 65 baada ya kipa Alexander Dominguez kuzidiwa ujanja na Richarlson.

Penalti ambayo refa Alexis Herrera aliwapa Brazil ilichangiwa na tukio la Jesus kuchezewa visivyo na beki Angelo Preciado ndani ya kijisanduku cha Ecuador.

Brazil wanajiandaa sasa kumenyana na Paraguay mjini Asuncion mnamo Juni 8 huku Ecuador wakialika Peru siku hiyo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Serikali kujenga daraja la Sh25 milioni kuokoa biashara za...

Magavana wadai Jubilee ina nia ya kuua ugatuzi