• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 3:46 PM
Budapest: Mtembeaji Gathimba akosa Sh720,000 kwa kumaliza nambari tisa 

Budapest: Mtembeaji Gathimba akosa Sh720,000 kwa kumaliza nambari tisa 

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA wa Afrika kutembea kwa haraka kilomita 20 mwaka 2016, 2018 na 2022, Samuel Gathimba ameridhika na nafasi ya tisa kwenye Riadha za Dunia nchini Hungary, Jumamosi.

Alvaro Martin kutoka Uhispania (1:17:32), Mbrazil Caio Bonfim (1:17:39) na Perseus Karlstrom (1:17:47) walinyakua dhahabu, fedha na shaba, mtawalia.

Gathimba ni Mkenya wa kwanza kati ya 49 kujitosa uwanjani jijini Budapest.

Fani hii iliyofaa kuanza saa tatu na dakika 50 saa za Kenya, ilicheleweshwa kwa saa mbili kutokana na mvua ya radi.

Gathimba aliyekuwa akilenga kupata medali amekamilisha umbali huo kwa saa 1:18:34. Watembeaji wanane wa kwanza walipokea tuzo. Inamaanisha Gathimba alikosa zawadi ya nafasi ya nane ya Sh721,000.

Nambari moja hadi tatu walituzwa Sh10.0 milioni, Sh5.0m na Sh3.1m, mtawalia.

Kutokana na mvua ya radi, matembezi hayo ya haraka ya kilomita 20 ya wanaume yalisukumwa mbele kwa saa mbili.

Gathimba ni mmoja wa Wakenya 49 wanaoshiriki makala haya ya 19 yaliyovutia zaidi ya washiriki 2,000 kutoka timu 200.

Anashikilia rekodi ya Afrika ya saa 1:18:23 aliyoweka ugani Kasarani mnamo Juni 18, 2021. Pia, Gathimba anashikilia pia rekodi ya Riadha za Afrika ya 1:19:24 kutoka makala ya 2016.

Mchina Jun Zhang, Mbrazil Caio Bonfim na Mjapani Koki Ikeda waliingia matembezi hayo wakijivunia muda ya tatu-bora mwaka 2023 baada ya kukamilisha umbali huo kwa 1:17:38, 1:18:29 na 1:18:36, mtawalia.

Gathimba naye alikuwa na 1:22:49, muda uliomweka katika nafasi ya 39 katika orodha ya washiriki 50.

Si mara ya kwanza Gathimba kushiriki Riadha za Dunia. Alimaliza nambari nne katika makala ya 2022 mjini Eugene, Amerika, nambari 33 mwaka 2019 (Qatar) na nambari 30 mwaka 2017 (Uingereza).

  • Tags

You can share this post!

Uswidi wakomoa wenyeji Australia na kujizolea nishani ya...

Chelsea wang’oa kiungo Romeo Lavia kutoka Southampton...

T L