• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 9:50 AM
Chelsea wapiga West Ham United na kuingia ndani ya nne-bora katika EPL

Chelsea wapiga West Ham United na kuingia ndani ya nne-bora katika EPL

Na MASHIRIKA

KOCHA Thomas Tuchel amesema Chelsea “watajiamini” sana dhidi ya Real Madrid kwenye gozi lao lijalo la nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kuwapepeta West Ham United 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi.

Ushindi huo wa Chelsea uliwaweka pazuri zaidi kukamilisha kampeni za muhula huu ndani ya orodha ya nne-bora jedwalini na hivyo kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Bao la Werner aliyesajiliwa kutoka RB Leipzig ya Ujerumani mwishoni mwa msimu uliopita lilikuwa lake la kwanza ndani ya jezi ya Chelsea tangu Februari 2021 na la sita kufikia sasa muhula huu ligini.

Goli lake dhidi ya West Ham lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na fowadi raia wa Amerika, Christian Pulisic.

Chelsea wameratibiwa kuvaana na Real katika mkondo wa kwanza wa UEFA mnamo Aprili 27 ugani Stamford Bridge, Uingereza kabla ya kurudiana ugani Alfredo Di Stefano, Uhispania wiki moja baadaye.

“Ushindi huu bila shaka ni kitu spesheli na ni ufanisi unaotupa motisha zaidi ya kuwaalika Real tukiwa na matumaini tele ya kuendeleza ubabe wetu. Real wametawala soka ya bara Ulaya kwa miaka 10 iliyopita na ni mabingwa mara 13 wa kipute cha UEFA, hivyo kibarua kilichopo mbele yetu si chepesi,” akasema Tuchel.

Pigo zaidi kwa West Ham ni kwamba walikamilisja mchuano huo dhidi ya Chelsea wakiwa na wanasoka 10 pekee uwanjani baada ya Fabian Balbuena kuonyeshwa kadi nyekundu na refa Chris Kavanagh kwa kosa la kumchezea visivyo beki Ben Chilwell katika dakika ya 81.

Chini ya kocha David Moyes, West Ham kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano kwa alama 55, tatu nyuma ya Chelsea wanaofunga mduara wa nne-bora. Hii ni baada ya Liverpool kulazimishiwa sare ya 1-1 katika mchuano wa awali dhidi ya Newcastle United ugani Anfield.

Tuchel alipotwaa mikoba ya Chelsea mnamo Januari 2021 baada ya kuaminiwa kuwa mrithi wa Frank Lampard, kikosi hicho kilikuwa kikishikilia nafasi ya tisa jedwalini. Lakini kwa sasa klabu hiyo imefuzu kwa fainali ya Kombe la FA itakayowakutanisha na Leicester City, wanafukuzia taji la UEFA na wanawania fursa ya kuwa miongoni mwa timu zitakazokamilisha kampeni za msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora.

West Ham kwa sasa wamesalia na mechi tano zaidi katika EPL msimu huu dhidi ya Burnley, Southampton, Brighton na West Brom kwa usanjari huo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

JAMVI: IEBC yawaniwa kutekwa nyara kabla ya kura 2022

Hospitali ya Tigoni yatoa hewa ya oksijeni bure kwa wagonjwa