• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
Clevers Kyalo: Kiungo mahiri mwenye ndoto ya kuchezea Wazito FC na klabu za ughaibuni

Clevers Kyalo: Kiungo mahiri mwenye ndoto ya kuchezea Wazito FC na klabu za ughaibuni

NA PATRICK KILAVUKA

MALENGO yake ni kucheza kama kocha Mhispania Xavi Hernández, 45, ambaye zamani alisakatia timu ya Barcelona ngarambe kabla ya kurejea baadaye na kuanza kuinoa.

Tunamzungumzia Clevers Kyalo,17, ambaye ni mweledi katika kumiliki safu ya kiungo kutokana na pasi zake za uhakika na kujua kuweka jicho kwa mpira na kuudhibiti akiwa ugani.

Kiungo huyu wa timu ya Makadara Youth yenye makao makuu Hamza, Kaunti ya Nairobi anajisuka kuhakikisha kwamba anavuta kamba yake ya kuwa mchezaji ambaye anaweza kuhimili makali na dhoruba za kusakata boli ili, afike kiwango cha mchezaji mtajika huyo huku akitilia maanani kwamba, siku za halafu anaweza kupenya kusakatia soka timu kama Barcelona ambayo anaienzi sana.

Kwa sasa kiungo Clevers ni mwanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Upili ya Upper Hill, Nairobi ambako pia kabumbu imezingatiwa kama njia ya kuinua vipaji vya kandanda mbali na masomo kupewa kipaumbele. 

Amechezea shule yake ya wasiozidi umri wa miaka 19 hadi mashindano ya kanda ya shule za upili za Kaunti ya Nairobi (KSSSA), ambayo yaliandaliwa katika Lenana School mwaka 2022.

Aidha, alifika kiwango sawa na hicho katika mashindano ya shule za msingi ambayo yaliandaliwa shule ya msingi ya Moi Forces, Nairobi akiwa shule ya msingi ya Mukuru kwa Njenga alikosomea.

Mwanasoka chipukizi Kyalo alianza kusakata boli akiwa na miaka tisa akiwa katika Darasa la Tano.

Uchezaji wake ulivutia timu kama Grand Spark ya Mradi, Tassia, Nairobi akaiwajibikia kabla kuhamia Bosco Sports Network (BSN).

Safari yake kisoka iliendelea kuwa shwari pale ambapo alichukuliwa na Shofco Mukuru kwa Njenga na kumpokeza masomo.

Mwanasoka Clevers Kyalo akifanya mazoezi. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Anasema ni wakati huo, kwa ushirikiano mwema na timu ya Makadara Youth, amepata kuinua talanta yake ya kugaragaza gozi kwani akiwa timu ya Youth amekumbatiwa vyema na wadau wengi wakiwemo kocha Walter Onyare na kocha wa makinda Kevin Odando ambaye ameshikilia akiwa anaichezea kuanzia U-10.

Mwanakandanda Clevers anasema alianza kwa kumuiga binamuye Lamek Anami ambaye anachezea Bidco FC.

Aidha Anami alikuwa anampa mshawasha wa kuenda kupiga zoezi naye kila siku.

Tayari Clevers ametuzwa kama mwanasoka bora katika kipute cha Jidhamini Tournment mihula miwili 2018 na 2019 mtawalia.

Mwaka huu ni wake wa kwanza kucheza katika kikosi cha kwanza cha timu ya Makadara Youth katika kingang’anyiro cha ligi ya Kanda ya FKF, Nairobi East (NERL). Alionyesha soka safi katika mchuano wao dhidi ya Hakati Sportiff ambao uliishia kwa wao kupigwa 1-0.

Mwanasoka Clevers Kyalo (wa tano kulia) kikosini Makadara Youth. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Anatazamia kusakata boli katika mashindano ya mwaka ya shule za upili ambapo shule yake itashiriki. Hata hivyo, kabla kushika rada na pengine kuwajibikia timu za ughaibuini, angependa kuchezea Wazito FC akisema wana mfumo mzuri wa uchezaji ambao unalandanada na uchezaji wake na matamanio yake kisoka.

Angependa kuwashukuru wadau wa timu yake na wazazi, Shofco Mukuru kwa Njenga, na mashabiki kwa sapoti ambayo wamempa kujikuza kisoka na masomo kwani ni fursa ambazo hawezi kuzichukulia hivi hivi.

Aidha, hayo yote anasema yanawezekana tu kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu aliyemruzuku talanta adhimu ambayo anasema itaweza kumfikisha mbali.

Ushauri wake kwa wanasoka chipukizi ni kwamba, kusakata boli kunahitaji ari na bidii na kwamba soka ni ajira.
  • Tags

You can share this post!

Wito kwa wenye uwezo wamsaidie mvulana aliyezoa 306 aingie...

Washukiwa wawili wakamatwa kwa kuuza pombe haramu na...

T L