• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Crystal Palace yamtimua kocha Patrick Vieira

Crystal Palace yamtimua kocha Patrick Vieira

NA MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA Patrick Vieira ameingia katika orodha ndefu ya makocha wa Ligi Kuu ya Uingereza walioangukiwa na shoka kutokana na msururu wa matokeo duni msimu huu.

Kupitia mwenyekiti Steve Parish, Crystal Palace, ambayo itavaana na viongozi Arsenal ugani Emirates mnamo Jumapili, ilithibitisha kufuta kazi Mfaransa huyo baada ya kumuajiri miezi 18 iliyopita, pamoja na wasaidizi wake Osian Roberts, Kristian Wilson na Said Aigoun. Dean Kiely atasalia kocha wa makipa.

Parish alitaja matokeo mabovu ambayo yameweka Palace hatarini kushushwa daraja kuwa sababu ya kufanya mabadiliko katika benchi ya kiufundi.

“Tunahisi kuwa mabadiliko yatatupatia nafasi nzuri ya kutetea hadhi yetu kwenye Ligi Kuu,” alisema na kupongeza Vieira kwa kusaidia Palace kufika nusu-fainali ya Kombe la FA na kumaliza Ligi Kuu katika nafasi ya 12 msimu uliopita.

Hata hivyo, Vieira hajaonja ushindi ligini mwaka 2023 ambapo Palace imepoteza michuano sita ligini ikiwemo tatu iliyopita bila kufunga bao na kutoka sare mara tano.

Rafa Benitez, Nuno Espirito Santo, Ange Postecoglu, Ralph Hassenhuttl, Mauricio Pochettino, Marcelo Bielsa, Steven Gerrard na Carlos Coberan ni makocha wanaopigiwa upatu kujaza nafasi ya Vieira.

Makocha 10 wa EPL sasa wamepoteza kazi msimu huu. Waliotangulia Vieira ni Scott Parker (Bournemouth), Thomas Tuchel (Chelsea), Bruno Lage (Wolves), Steven Gerrard (Aston Villa), Hasenhuttl (Southampton), Frank Lampard (Everton), Jesse Marsch (Leeds) na Nathan Jones (Southampton).

Makocha wengine wanaoning’inia pabaya ni Brendan Rodgers (Leicester), David Moyes (West Ham), Ruben Selles (Southampton), Gary O’Neil (Bournemouth) na Antonio Conte (Tottenham). Palace na Arsenal watakuwa na presha kupata ushindi mnamo Jumapili.

Mechi hii itawapa wanabunduki wa Arsenal fursa ya kuongeza mwanya kati yao na nambari mbili Manchester City hadi alama nane.

Mabingwa watetezi City hawana mechi ya ligi wikendi hii kwa sababu ya majukumu ya Kombe la FA ambapo ni wenyeji wa Burnley katika robo-fainali.

Ratiba

EPL

Machi 18 – Brentford v Leicester (6.00pm), Southampton v Tottenham (6.00pm), Aston Villa v Bournemouth (6.00pm), Wolves v Leeds (6.00pm), Chelsea v Everton (8.30pm);

Machi 19 – Arsenal v Crystal Palace (5.00pm).

Kombe la FA

Machi 18 – Manchester City v Burnley (8.45pm); Machi 19 – Sheffield United v Blackburn Rovers (3.00pm), Brighton v Grimsby Town (5.15pm), Manchester United v Fulham (7.30pm).

  • Tags

You can share this post!

BORESHA AFYA: Vyakula vinavyoweza kuongeza serotonini...

MAPISHI KIKWETU: Keki ya kahawa na tufaha

T L