• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 3:46 PM
De Bruyne na Lukaku waongoza Ubelgiji kupepeta Wales katika gozi la kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022

De Bruyne na Lukaku waongoza Ubelgiji kupepeta Wales katika gozi la kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022

Na MASHIRIKA

WANASOKA Kevin De Bruyne, Thorgan Hazard na Romelu Lukaku walisaidia Ubelgiji kutoka nyuma na kuzamisha chombo cha Wales 3-1 katika mechi ya ufunguzi wa kampeni za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Chini ya unahodha wa Gareth Bale wa Real Madrid anayechezea Tottenham Hotspur kwa mkopo, Wales waliwekwa uongozini na Harry Wilson baada ya kushirikiana vilivyo na Connor Roberts katika dakika ya 10.

Goli la Wales liliwazindua Ubelgiji wanaoshikilia nafasi ya kwanza duniani kwa mujibu wa orodha ya viwango bora vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

De Bruyne ambaye ni kiungo wa Manchester City nchini Uingereza, aliwasawazishia Ubelgiji katika dakika ya 22, dakika sita kabla ya Hazard wa Borussia Dortmund nchini Ujerumani kufunga bao la pili.

Lukaku anayechezea Inter Milan ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A), aliwafungia Ubelgiji bao la tatu katika dakika ya 73 kupitia mkwaju wa penalti.

Kichapo hicho kilikuwa cha kwanza kwa Wales kupokea tangu Juni 2019, matokeo yaliyokomesha rekodi ya kitaifa ya kutoshindwa katika jumla ya mechi 11 mfululizo.

Wales waliokuwa wakichezea ugenini, wanawania fursa ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1958.

Wakijivunia rekodi ya kutoshindwa nyumbani tangu 2010, Ubelgiji ni miongoni mwa mataifa yanayopigiwa upatu wa kutawazwa mabingwa wa Kombe la Dunia la 2022.

Mara ya mwisho kwa Wales kushinda Ubelgiji ni kwneye robo-fainali za Euro 2016 ambapo miamba hao walipokezwa kichapo cha 3-1.

Tangu wakati huo, Ubelgiji wamefunga jumla ya mabao 153 katika jumla ya michuano 51 chini ya kocha wa zamani wa Everton, Roberto Martinez.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kampuni yashtakiwa kwa kuharibu mti wa Raila

Mkondo wa kunifurusha Jubilee hauna faida – Ruto