• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Everton waangusha Chelsea katika EPL ugani Goodison Park

Everton waangusha Chelsea katika EPL ugani Goodison Park

NA MASHIRIKA

EVERTON waliweka hai matumaini ya kusalia katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) muhula ujao kwa msimu wa 69 baada ya kupiga Chelsea 1-0 uwanjani Goodison Park mnamo Jumapili.

Chini ya kocha Frank Lampard, Everton walianza mechi wakiwa na ulazima wa kuangusha miamba Chelsea ili kukwepa shoka ambalo vinginevyo lingewaweka katika hatari ya kuungana na Norwich City ambao tayari wameteremshwa ngazi kwenye EPL msimu huu.

Everton sasa wanakamata nafasi ya 18 kwa alama 32 huku pengo la pointi 10 likitamalaki kati yao na nambari 19 Watford. Nafuu zaidi kwa Everton ni kwamba wametandaza mechi 33, moja chini ya Leeds United na Burnley wanaojivunia alama 34 kila mmoja.

Bao la Everton dhidi ya Chelsea lilipachikwa wavuni na fowadi Richarlson Andrade aliyemzidi ujanja beki na nahodha Cesar Azpilicueta mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Kufikia sasa, Everton wameshinda mechi tisa, kuambulia sare mara tano na kupoteza michuano 19 katika EPL msimu huu. Kikosi hicho kinachonolewa na mchezaji na mkufunzi wa zamani wa Chelsea, kilipokezwa na Liverpool kichapo cha 2-0 katika mechi yao ya awali katika EPL huku Chelsea wanaoshikilia nafasi ya tatu kwa alama 66 wakiambulia sare ya 1-1 dhidi ya Man-United ugani Old Trafford.

Mara ya mwisho ambapo Everton walianza mechi ya EPL wakiwa miongoni mwa vikosi vitatu vya mwisho, walijinyanyua na kucharaza Chelsea 3-1 ugani Goodison Park mnamo Disemba 2019. Chelsea waliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Everton walipokutana katika mkondo wa kwanza wa EPL msimu huu ugani Stamford Bridge mnamo Disemba 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kaunti yafunza wauguzi wake kutambua kansa

Wafanyikazi wanaopata mishahara duni wapewa nyongeza ya...

T L