• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
FIFA yagonga Gor kiboko cha miaka 2 kwa sababu ya jeuri

FIFA yagonga Gor kiboko cha miaka 2 kwa sababu ya jeuri

Na CECIL ODONGO

KWA mara nyingine, vigogo wa soka nchini Gor Mahia wamejipata pabaya baada ya kuangushiwa marufuku ya kutowasajili wachezaji wapya hadi kipindi cha uhamisho wa wachezaji mnamo 2023.

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) lilichukua hatua hiyo mnamo Jumatatu usiku baada ya timu hiyo kupatikana na hatia ya kuwanunua na kuwasajili wachezaji ilhali ilikuwa ikitumikia marufuku nyingine ya Fifa.

‘Klabu hii imepatikana na hatia ya kukosa kutii sheria za fifa,’ barua kutoka kitengo cha Kutatua Mizozo iliyotiwa saini na Paola Lopez Baraza kutoka Mexico kwa niaba ya Fifa.’Klabu hii ya Gor Mahia imepigwa marufuku ya kuwasajili wachezaji wapya kwa vipindi viwili vinavyofuatana kutoka tarehe ambayo uamuzi huu umetolewa,’ ikaongeza barua hiyo.

Isitoshe, Fifa pia iliangushia FKF adhabu kali ya faini ya Sh6 milioni kwa kuwasajili wachezaji hao na kuwaruhusu waichezee K’Ogalo. Iliweka wazi kuwa faini hiyo italipwa na FKF ndani ya siku 30 zijazo. Mwezi uliopita, Fifa ilianzisha mchakato wa kuiadhibu Gor na FKF baada ya timu hiyo kuwachezesha Sando Yangaya, Dennis Ng’ang’a, na Peter Lwassa katika kipute cha ufunguzi wa msimu mpya wa Super Cup dhidi ya Tusker mnamo Septemba 22.

Hii ni licha ya kwamba Fifa ilikuwa imewapiga marufuku ya kuwasajili wachezaji wapya kwa kukosa kukamilisha malipo ya waliokuwa wanasoka wake Shafiq Batambuze na Dickson Ambudo pamoja na aliyekuwa kocha wao Steven Polack.

Habari hizi ni pigo kwa kocha Mark Harrison ambaye ameanza msimu huu vizuri akiwa kocha wa K’Ogalo. Mababe hao wanaongoza ligi kwa alama 14 na hawajapoteza mechi yoyote msimu huu baada ya kujibwaga uwanjani mara sita.

Mbali na hayo, Gor inashiriki mashindano ya Kombe la Mashirikisho Afrika CAF) ambapo imeratibiwa kuchuana na As Otoho d’Oyo ya Jamuhuri ya Congo baadaye mwezi huu.Fifa pia imefunga faili ya kesi ambapo aliyekuwa kocha wa Harambee Stars Adel Amrouche alikuwa ameishtaki FKF kwa kutomlipa malimbikizi ya mishahara yake.

Hii ni baada ya Amrouche kulipwa pesa zake zote na FKF.

You can share this post!

Hakuna kupimwa wazimu kwa washukiwa wa mauaji

Ulinzi Starlets imani tele taji lao

T L