• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
Harambee Stars yalenga Misri baada ya mechi ya kirafiki dhidi ya TZ kuondolewa

Harambee Stars yalenga Misri baada ya mechi ya kirafiki dhidi ya TZ kuondolewa

NA GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Stars imetupia jicho mchuano wa kufuzu kushiriki Kombe la Afrika dhidi ya Misri baada ule wa kirafiki dhidi ya Tanzania kufutiliwa mbali Alhamisi kutokana na kifo cha Rais John Pombe Magufuli.

Vijana wa Jacob ‘Ghost’ Mulee walifaa kumenyana na Taifa Stars katika mechi ya pili ya kupimana nguvu baada ya kushinda ile ya kwanza 2-1 Machi 15. Rais Magufuli aliaga dunia Machi 17 usiku.

Harambee Stars na Taifa Stars zilikuwa zimekubali kuendelea na mechi hiyo zikipanga kuianza kwa kunyamaza dakika moja.

Hata hivyo, mashirikisho ya soka ya nchi hizo mbili FKF na TFF yalitoa habari Alhamisi yakisema kuwa mchuano huo umefutwa.

Kenya, ambayo ililemea Sudan Kusini 1-0 katika mechi nyingine ya kirafiki Machi 13, itaalika Misri katika uga wa kimataifa wa Kasarani mnamo Machi 25 katika mechi yake ya tano ya Kundi G.

Vijana wa Mulee wanashikilia nafasi ya tatu kwenye kundi hilo wakiwa na matumaini finyu ya kufuzu. Misri na wanavisiwa wa Comoros wako sako kwa bako katika nafasi mbili za kwanza kwa alama nane.

Wakenya wataelekea jijini Lome kukamilisha kampeni yao dhidi ya Togo mnamo Machi 29.

Aidha, Mafirauni wa Misri walitaja Alhamisi kikosi chao cha wachezaji 28 kwa michuano yao mbili ya mwisho dhidi ya Kenya na Misri.

Kikosi cha kocha Hossam El-Badry kina nyota Mohamed Salah (Liverpool, Uingereza) na Mohamed Elneny (Arsenal).

Hiki hapa kikosi kizima cha Misri:

Makipa – Mohamed El-Shennawy (Al Ahly), Mahmoud Gennesh (Zamalek), Mohamed Bassam (Tala’a El-Gaish), Amer Amer (Ceramica Cleopatra);

Mabeki – Mohamed Hany, Ayman Ashraf, Yasser Ibrahim (Al Ahly), Omar Gaber, Ali Gabr, Ahmed Ayman Mansour (Pyramids), Ahmed Fetouh, Mahmoud El-Wensh (Zamalek), Ahmed Hegazi (Ittihad Jeddah);

Viungo – Mohamed Elneny (Arsenal), Amr El-Sulya, Hamdi Fathi, Mohamed Magdy Afsha (Al Ahly), Tarek Hamed, Ahmed Sayed Zizo (Zamalek), Mohamed Salah (Liverpool), Mahmoud Trezeguet (Aston Villa), Mohamed Farouk, Islam Issa (Pyramids), Mostafa Fathi (Smouha);

Washambuliaji – Mostafa Mohamed (Galatasaray), Hossam Hassan (Smouha), Ahmed Yasser Rayan (Ceramica Cleopatra), Mohamed Sherif (Al Ahly).

  • Tags

You can share this post!

Spika wa Bunge la Tanzania awaita wabunge Dodoma

Oliver Solberg halali akiota kufuata nyayo za babaye Petter...