• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 2:00 PM
Hatimaye Nzoia waonja raha ya ushindi Ligi Kuu

Hatimaye Nzoia waonja raha ya ushindi Ligi Kuu

Na CECIL ODONGO

WANASUKARI wa Nzoia Sugar jana walijizolea ushindi wao wa kwanza katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL) msimu huu, huku Kenya Police ikitoka sare ya 1-1 na Wazito FC katika uga wa kitaifa wa Nyayo.

Katika mechi nyingine ya jana Mathare United ililambishwa sakafu 2-0 na Nairobi City Stars ugani Ruaraka. Ugani Sudi, Nzoia ilifunga Kariobangi Sharks 3-1 huku ikitawala mechi nzima kumpunguzia presha Kocha Ibrahim Shikanda, ambaye alikuwa ametishia kujiuzulu kutokana na matatizo tele ya kifedha yanayoikumba timu hiyo.

Mshambuliaji Levis Okello alifungia Nzoia mabao yote, huu ukiwa msimu wake katika ligi kuu baada ya kujiunga na timu hiyo kutoka Vihiga Bullets mnamo Oktoba.Okello alifunga bao kipindi cha kwanza kisha kuongeza mengine kipindi cha pili, mara nyingi akiwazidi ujanja mabeki wa Sharks kisha kumbwaga vibaya mnyakaji wao Brandon Obiero.

Bao pekee la Sharks lilitiwa wavuni na Erick M’mata dakika ya 21 baada ya Randy Bakari kunawa mpira ndani ya kijisanduku.Ugani Nyayo, Duke Abuya alifungia Kenya Police kupitia shuti kali dakika ya 40 baada ya kumegewa pasi safi na chipukizi Clinton Kinanga.

Hata hivyo, Wazito yake Francis Kimanzi ilisawazisha dakika ya 55 huku Duncan Otieno akijifunga akijaribu kuokoa mpira hatari na kuwanyima Kenya Police ushindi wa pili mfululizo baada ya kuilemea Sharks 3-1 katikati mwa wiki.Nayo Nairobi City Stars ilirejelea ushindi kwa kuipiku Mathare United 2-0.Peter ‘Pinchez’

Opiyo alifunga mabao yote mawili kipindi cha kwanza kukomesha mtindo wa kukosa ushindi katika mechi mbili zinazofuatana.Aliyatinga mabao hayo dakika ya 19 kupitia mpira wa ikabu uliochanjwa vizuri kisha kujaza wavuni mpira baada ya kugeuka na kuwapita mabeki wa Mathare United.

Kocha wa Nzoia, Ibrahim Shikanda, aliwataka vijana wake watumie ushindi huo kama motisha kukabili wapinzani katika mechi zao zijazo.“Ushindi huu sasa ufungue mlango wa matokeo mazuri katika mechi zijazo. Tunafaa kujituma sana mazoezini na pia kuweka bidii katika mechi zetu.

“Tatizo letu limekuwa kufunga lakini nashukuru leo tulipata bao na kutumia vyema mechi zetu,” akasema Shikanda.Leo ubabe wa nani atasalia kileleni utashuhudiwa huku viongozi wa ligi Gor Mahia na nambari mbili Kakamega Homeboyz, wakiwa na kibarua kigumu dhidi ya Bandari na Bidco United mtawalia.

AFC Leopards watasaka ushindi wao watatu wakipambana na wavuta mkia Vihiga Bullets. Leopards ilipiga Posta Rangers 1-0 mnamo Alhamisi.RATIBA (Leo):

Gor Mahia vs Bandari (Kasarani, 3pm)Posta Rangers vs FC Talanta (Thika Stadium, 3pm)Vihiga Bullets vs AFC Leopards (Bukhungu Stadium, 1pm)Tusker vs Sofapaka (Ruaraka Grounds, 3pm)KCB vs Ulinzi ( Utalii Grounds, 3pm)

You can share this post!

Leicester, West Ham na Everton mawindoni EPL

Patashika Madrid! Real na Atletico kutifua kivumbi

T L