• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:15 PM
Hellen Obiri alenga kutetemesha kwenye New York City Marathon

Hellen Obiri alenga kutetemesha kwenye New York City Marathon

Na AYUMBA AYODI

BINGWA wa Boston Marathon, Hellen Obiri amesisitiza hatashiriki Riadha za Dunia nchini Hungary mwezi Agosti na badala yake atatimka New York City Marathon mnamo Novemba 5.

Mshindi huyo wa Riadha za Dunia mbio za 5,000 mwaka 2017 na 2019 Obiri alifichua hayo baada ya kunyakua taji lake la nne la mbio za mita 5,000 kwenye riadha za majeshi (KDF) uwanjani Ulinzi Sports Complex mnamo Jumatano.

Obiri, ambaye pia alishinda taji la KDF la 5,000m mwaka 2016, 2017 na 2021, alimlemea mshindi wa nishani ya shaba ya Jumuiya ya Madola mbio za 10,000m Selah Jepleting katika mita 200 za mwisho.

Ushindani mkali ulikuwa kati ya Obiri, Jepleting na Cythia Chepng’eno ikisalia mizunguko minne.

Obiri na Jepleting walibadilishana uongozi mara kadhaa kabla ya Obiri kufyatuka mita 200 za mwisho na kutwaa taji kwa dakika 15:19.70.

Jepleting na Chepng’eno waliridhika na nafasi mbili zilizofuata kwa 15:21.36 na 15:23.36, mtawalia.

“Nilihisi vizuri kujituma vilivyo kwa sababu Jepleting hakunipa nafasi ya kupumua,” akasema Obiri aliyeshinda mbio za kilomita 10 za Great Manchester Run wikendi iliyopita.

“Sikuwa nimeshiriki mashindano hapa nyumbani kwa karibu mwaka mzima kwa hivyo niliamua kuja hapa na kuwakilisha timu yangu ya Laikipia Air Base pamoja na kutetea taji langu,” aliongeza Obiri.

“Mbio za uwanjani mara nyingi hunisaidia kutafuta kasi ninayohitaji katika marathon.”

Obiri alianza maisha yake katika Marathon Kuu Duniani (WMM) kwa kukamata nafasi ya sita kwenye New York City Marathon mwaka 2022 kwa saa 2:25:49.

Kisha, Obiri alitwaa taji la Boston Marathon kwa 2:21.38 mnamo Aprili 17, 2023 kabla ya kuhifadhi ubingwa wa Manchester Great Run.

“Nilivyosema hapo awali ni kuwa sitakuwa Budapest, Hungary kwa sababu bado sijaiva kuwakilisha taifa katika marathon kwenye Riadha za Dunia,” alieleza Obiri.

Taji la KDF la wanaume la 5000m liliendea mshindi wa medali ya fedha ya Riadha za Nusu-Marathon Duniani Kibiwott Kandie aliyekata utepe kwa dakika 28:19.32 baada ya kuwatoka wapinzani wake ikisalia mizunguko minane.

Kandie, ambaye alikuwa nambari nne kwenye Mbio za Nyika Duniani nchini Australia mwezi Februari, alifuatwa kwa karibu na Hillary Koech (28:35.20) na Abel Mutai (28:43.76).

Kandie alifichua kuwa lengo lake ni kuwa katika timu ya Kenya itakayoshiriki Riadha za Dunia nchini Hungary baada ya kukosa makala ya 2022 jimboni Oregon, Amerika.

  • Tags

You can share this post!

IPOA yaanzisha uchunguzi baada ya polisi kuua raia sita...

Hii imeenda! Ben White na Milly sasa ni mtu na mkewe

T L