• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Hit Squad ya Kenya yamaliza nambari 12 mashindano ya Afrika

Hit Squad ya Kenya yamaliza nambari 12 mashindano ya Afrika

Na AYUMBA AYODI

KENYA ilikamilisha makala ya 12 ya mashindano ya ndondi ya Afrika katika nafasi ya 12 baada ya Nick “Commander” Okoth, Samuel Njau na Elizabeth Andiego kuzoa medali za fedha naye Boniface Mogunde akashinda shaba mjini Maputo, Msumbiji.

Matumaini ya Kenya, ambayo ilikamata nafasi ya nane baada ya kuzoa dhahabu kupitia kwa Okoth na shaba kutoka kwa Shaffi Bakari, John Kyalo, Christine Ongare na Elizabeth Akinyi katika makala yaliyopita nchini Congo Brazzaville mwaka 2017, kupata dhahabu mjini Maputo yalizimwa wakati Okoth, Njau na Elizabeth Andiego walipigwa katika fainali Septemba 17.

Wenyeji Msumbiji ni wafalme wapya wa Afrika baada ya kuzoa dhahabu tano na shaba mbili.

Algeria (dhahabu nne, fedha tano na shaba sita), Zambia (dhahabu nne na shaba tatu), Morocco (dhahabu mbili, fedha tano na shaba mbili) na Camaeroon na DR Congo (dhahabu mbili, fedha tatu na shaba nne kila mmoja) walikamilisha nafasi tano za kwanza kwenye mashindano hayo yaliyovutia mataifa 18.

Timu ya taifa ya Kenya almaarufu Hit Squad ilijumuisha mabondia wanane.

Kwa mara ya kwanza kabisa, Shirikisho la Ndondi Afrika (AFBC) lilitunuku wanamedali zawadi ya kifedha.

Okoth alipoteza taji mikononi mwa Andrew Chilata kutoka Zambia kwa wingi wa alama katika uzani wa kilo 60 (Light).

Njau, ambaye alikuwa akishiriki mashindano haya kwa mara ya kwanza kabisa, alicheza raundi zote akipoteza dhidi ya Rugoberto Sigauque katika uzani wa kilo 57 (Feather).

Andiego alipatia Kenya medali ya kwanza ya fedha aliposalimu amri ya Khadija Mardi kutoka Morocco katika uzani wa zaidi ya kilo 81 (Heavy).

Mogunde alikuwa ameridhika na shaba ya uzani wa kilo 71 (Middle) mnamo Septemba 15.

Washindi wa medali ya dhahabu walipokea tuzo ya Sh1.2 milioni, fedha wakatia mfukoni Sh600,000 nao waliopata shaba wakazawadiwa Sh300,000.

Bakari (bantam) na Ongare (minimum) walibanduliwa katika robo-fainali nao Amina Martha (bantam) na David Karanja (fly) walipanguliwa katika raundi ya kwanza.

Kocha mkuu Benjamin Musa alisema si matokeo walitarajia, lakini anafurahia matokeo waliyopata kutokana na kikosi hicho kidogo.

“Tulitamani sana kupata angaa dhahabu mbili, lakini Njau kukosa uzoefu dhidi ya mpinzani wake mzoefu Armando Sigauque kutoka Msumbiji kulitunyima dhahabu,” alisema Musa.

Alikiri kuwa watahitaji kutafutia wachezaji wapya mashindano ya kuwapatia uzoefu ili kupunguza mwanya kati ya Kenya na mataifa makubwa katika ndondi barani Afrika.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE 

  • Tags

You can share this post!

Kipchoge alenga rekodi Berlin Marathon

Mwanatenisi Ahoya aaga mashindano ya Afrika ya kwanza...

T L