• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:01 AM
Ighalo apata hifadhi Saudia

Ighalo apata hifadhi Saudia

Na MASHIRIKA

FOWADI Odion Ighalo amejiunga na kikosi cha Al Shabab nchini Saudi Arabia baada ya kipindi chake cha mkopo kambini mwa Manchester United kukamilika.

Mchezaji huyo raia wa Nigeria alikuwa akichezea Man-United kwa mkopo kutoka kambini mwa Shanghai Shenhua ya China.

Ighalo, 31, alirejea China mwishoni mwa Januari 2021 kabla ya kupata hifadhi kambini mwa Al Shabab ambao kwa sasa watakuwa wakimpokeza mshahara wa Sh18 milioni kwa wiki.

Kufikia sasa, Al Shabab wanadhibiti kilele cha jedwali la Ligi Kuu ya Saudi Arabia baada ya nusu ya mechi za kampeni ya msimu huu kusakatwa.

Ni matarajio ya usimamizi wa Al Shabab kwamba Ighalo atawasaidia kutia kapuni ubingwa wa Ligi Kuu ya Saudi Arabia kwa mara ya kwanza tangu 2012.

Akiwa Man-United, Ighalo alifungia The Red Devils mabao matano pekee kutokana na mechi 23. Kwa sasa atashirikiana na nyota wa zamani wa Sevilla, Ever Banega, kuongoza safu ya mbele ya Al Shabab.

“Nitashukuru usimamizi wa Man-United siku zote kwa fursa hii adimu waliyonipa kuvalia jezi za klabu ambayo nimekuwa nikiishabikia tangu utotoni. Nitasalia kuwa shabiki mkuu wa Man-United popote nitakapokuwa,” akaandika fowadi huyo kwenye mtandao wake wa Twitter.

Tangu atue guu kambini mwa Man-United, Ighalo amewajibishwa katika jumla ya michuano tisa pekee ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na nafasi yake katika kikosi cha kwanza ilitwaliwa kabisa na nyota Edinson Cavani aliyesajiliwa kutoka Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa mnamo Oktoba 2020.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wasiwasi Ghana wabunge 15 wakiugua corona

Kenya iliporwa Sh330.5 milioni ikipoteza pia uenyeji wa...