• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:50 AM
Joylove inataka kushiriki kipute cha CAF miaka ijayo

Joylove inataka kushiriki kipute cha CAF miaka ijayo

Na JOHN KIMWERE
TIMU za michezo huanzishwa kwa madhumuni tofauti ikiwamo kukuza vipaji vya chipukizi ili kuibuka wachezaji wa kimataifa miaka ijayo.
Klabu nyingi za soka la wanawake na wanaume nyakati zote hushiriki mchezo huo zikipania kufuzu kushiriki Ligi Kuu pia mashindano ya haiba kubwa duniani. Pia kinyume na miaka iliyopita michezo imeibuka kitenga uchumi ambapo vikosi vingi hunoa makucha ya wachezaji wao wakilenga wakomae ili kusajiliwa na klabu za kigeni.
Timu ya wasichana ya Joylove Academy iliyoshushwa daraja msimu uliyopita tayari imeonyesha inataka kurejea kushiriki ngarambe ya juu msimu ujao. Kikosi hiki cha kocha, Joyce Achieng tayari kimetwaa tiketi ya kushiriki fainali za kutafuta bingwa wa kaunti ya Kiambu kwa timu za ngarambe ya Regional League.
Wasichana hao tayari wanaongoza kwenye jedwali la Kundi A Kaunti Ndogo ya Kiambu wakifuatiwa na Gikambura Starlets. ”Sina shaka kutaja kuwa wachezaji wangu wameonyesha kuwa wamepania kurejea kushiriki mechi za Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza.
Tumebakisha fainali hatua mbili tu tutwae tiketi ya kupandishwa ngazi,” kocha huyo anasema na kuongeza kuwa ameandaa kikosi imara kufanya kweli kwenye mchezo wa mwisho katika ratiba ya muhula huu kabla washiriki fainali mbili za kuwania tiketi ya kupandishwa ngazi.
LOVE:Timu ya Joylove FC…Picha/ JOHN KIMWERE
Anawapa pongezi tele kwa kujituma mithili ya mchwa na kukaa kileleni mwa jedwali bila kupoteza mchezo wowote wala kutoka nguvu sawa. Kando na mafanikio mengine pia itakuwa furaha yangu kuona baadhi ya wachezaji wakiiva na kubahatika kuteuliwa kuchezea timu za taifa Harambee Starlets kwa wasiozidi umri wa miaka 17, miaka 20 na wakomavu.
Kadhalika anawashauri wachezaji wanaokuja kuwa nyakati zote lazima waonyeshe nidhamu nzuri ndani na nje ya uwanja.
NGARAMBE YA CAF
Katika mpango mzima kocha huyo anasema wamepania kukaza buti huku wakilenga kutwaa tiketi ya kufuzu kushiriki Ligi Kuu ya Soka la Wanawake (KWPL) ndani ya miaka mitatu ijayo.
Kadhalika anadokeza wanataka kuweka mikakati kabambe kuhakikisha wameshinda ubingwa wa Ligi Kuu pia taji la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ili kupata tiketi ya kuwakilisha Kenya katika mashindano ya Shirikisho la Afrika (CAF).
KIMATAIFA
”Sekta ya michezo nchini inahitaji ufadhili ili wahusika kupata nafasi nzuri kuendeleza jukumu la kunoa chipukizi wanaokuja. Sina budi kutaja kuwa ufadhili umeibuka donda sugu kwa timu nyingi za michezo mbali mbali.
Anatoa wito kwa wahisani wajitokeze na kusapoti timu za michezo mashinani ili kutimiza malengo ya wanasoka wengi ambao hutamani kushiriki soka la kulipwa ughaibuni.
Timu hii ilianzishwa mwaka 2015 na tayari imebahatika kunoa makucha ya vigoli wachache akiwamo Vivian Awuor (Kibera Soccer Ladies) na Nancy Wafula (Soccer Sisters) za Ligi Kuu (KWPL) na Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza mtawalia.
Vipusa hao wanajivunia kuibuka mabingwa wa Ligi ya Kaunti Ndogo ya Mkoa wa Kati bila kudondosha mechi yoyote pia kutawazwa wababe wa ngarambe ya CRL mwaka 2018.
Timu hii imeundwa na wachezaji wafuatao: Sharon Khasandi (kipa na nahodha), Beryn Migalusha  na  Vella Chairo (wasaidizi wa nahodha), Halima Melisa, Farida Wambui, Consolata Mbechi, Faith Achieng na Snorine Anzika.
Pia wapo Ruth Wekesa, Cynthia Atieno, Resah Naliaka, Bethel Aluoch na Patience Khasiala. Pia wapo Mercy Ayuma, Lilian Muthoni, Eunice Bosibori, Vella Chairo, Ruth Nekesa, Cynthia Zindori,  Brenda Atieno, Phanice Ayuma, Juliana Mwende na Mercy Nekesa.
  • Tags

You can share this post!

Chipukizi Appiah aanza kuona matunda ya uigizaji

Escalators imepania kushiriki ligi kuu ya Kenya miaka...

T L