• Nairobi
 • Last Updated November 28th, 2023 7:53 PM
Kayange: Shujaa wa 7s aliyewasha msisimko wa raga nchini na kote duniani

Kayange: Shujaa wa 7s aliyewasha msisimko wa raga nchini na kote duniani

NA GEOFFFREY ANENE

HUMPHREY ‘Tall’ Kayange ni mmoja wa mashujaa wa Kenya katika raga.

Mwanafunzi huyo wa zamani wa shule za msingi za Joseph Kang’ethe (Nairobi) na Hermann Gmeiner (Eldoret), shule ya upili ya St Peter’s Mumias (Kakamega) na vyuo vikuu vya Jomo Kenyatta (JKUAT) na Bristol (Uingereza) alichezea timu ya taifa ya Kenya kutoka mwaka 2004 hadi 2016.

“Nilikuwa nacheza soka nilipojiunga na St Peter’s Mumias katika Kidato cha Kwanza. Nilikuwa straika. Hata hivyo, nilipata wanasoka wengi sana katika shule hiyo na sikufanikiwa kuingia timu ya shule,” alitanguliza kuhusu safari yake ya michezo.

Aliingilia raga kiajali baada ya kupata wachezaji wakifanya mazoezi akiwa anatembea na rafiki yake wakati wa michezo jioni shuleni.

“Tulijiambia tujaribu raga tuone itatufikisha wapi. Sikuwa najua chochote kuhusu raga. Kutoka muhula wa pili, nilianza kucheza raga nikaifurahia,” akaeleza.

Kayange aliendeleza mchezo huo alipojiunga na Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta.

Hata hivyo, alitilia mkazo zaidi masomo kwa sababu raga haikuwa imepata umaarufu sana chuoni humo.

Baada ya miaka hiyo minne, Kayange alifuzu na shahada ya kwanza katika Bayokemia akizamia Biolojia ya Molekuli.

“Kisha nikaanza kutafuta kazi ili nipate unga. Baadaye nilijiunga na klabu ya raga ya Ulinzi ambapo sasa nikaanza kuchukulia raga kwa uzito,” akasimulia.

Kayange alichezea Ulinzi kwa miaka miwili, ilipovunjiliwa mbali akajiunga na ndugu yake Collins Injera katika klabu ya Mwamba, ambayo ndiyo alichezea hadi alipostaafu.

Mkenya Humphrey Kayange (kushoto) ampita mwanaraga wa Chile Pablo Mainguyague (kulia) na kufunga trai to mjini San Diego, jimbo la California nchini Amerika mnamo Februari 9, 2008. PICHA | MAKTABA

Kati ya changomoto alizokumbana nazo alipoanza kucheza raga ni kuwa, mchezo huo haukuwa maarufu na hata wazazi wake walionekana kuwa na tashwishi.

“Kwa sababu raga ni mchezo wa kugongana, kuna vitu unastahili kuwa navyo: uwe na mwili wenye misuli tinginya, daluga na mavazi maalum. Mwanzoni, tulitumia tishati za kawaida ambazo ziliraruka siku iyo hiyo! Ni baadayendipo tulipata uwezo wa kununua nguo rasmi za raga ambazo haziraruki kwa urahisi,” aeleza Kayange na kukiri haikuwa rahisi kuchanganya michezo na masomo.

“Kufaulu katika vitu hivi viwili, anasema, lazima utilie mkazo vyote kwa kutenga muda unaofaa kwa kila moja kuhakikisha hakuna inayotelekezwa,” aliongeza.

“Ukitoka mazoezi ya raga huwa umechoka kwa sababu ni magumu. Unataka kupumzika, lakini unakumbuka kesho unafaa kuwasilisha kazi ya darasani ama kuna mtihani unahitaji kusomea. Saa nyingine unasema huendi mazoezi kwa sababu ni wiki ya mtihani. Lazima upange wakati wako vizuri kwa sababu usipofanya hivyo utapata uko sawa kwa moja na kupoteza nyingine. Lazima chipukizi wanaojitosa katika mchezo huu wajue kuna maisha baada ya uchezaji. Kwa hivyo, wawekeze pia katika masomo,” anahoji.

Alipoanza raga shujaa wake alikuwa mchezaji Jonah Lomu kutoka New Zealand na Johnny Eales wa Australia.

“Kwa Eales nilijiona kabisa kwa sababu alikuwa mchezaji mrefu. Nilisema nataka kuwa kama wachezaji hao wawili ambao niliwaona kupitia runinga. Wakati huo, sikuwa nafikiria naweza kufika katika timu ya taifa. Pia, nilienzi uchezaji wa wachezaji kadhaa kutoka Kenya akiwemo Edward Rombo walionitia motisha sana,” akasema.

Matukio muhimu

 • Alistaafu Oktoba 2016 baada ya kushiriki mashindano mawili ya Kombe la Dunia la raga ya wachezaji saba kila upande, Olimpiki moja na Michezo ya Jumuiya ya Madola mara mbili.
 • Alichezea Kenya Shujaa misimu 12 katika Raga za Dunia na kushinda duru ya Singapore Sevens mwaka 2016.

“Nakumbuka pia tulikosa pembamba kuingia Kombe la Dunia la wachezaji 15 kila upande mwaka 2015 baada ya kumaliza Kombe la Afrika mwaka 2014 katika nafasi ya tatu kwa tofauti ya ubora wa magoli dhidi ya Namibia na Zimbabwe,” anasema.

 • Alikuwa balozi wa Shirikisho la Raga Dunia wa masuala ya vita dhidi ya matumizi ya pufya mwaka 2010 na pia kusaidia sana katika raga ya wachezaji saba kila upande kujumuishwa kwenye Olimpiki.
 • Mwanasayansi huyo anafanya kazi katika Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Nchini (KEBS) idara ya utafiti na maendeleo.

“Akilini mwangu, nilitaka kuchukua mapumziko katika raga baada ya kustaafu kwa sababu nilikuwa nimecheza kwa miaka mingi,” akasema Kayange.

 • Alianza kusomea ukocha, lakini akapata fursa ya kuingia katika Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki nchini Kenya (NOC-K) kama mwakilishi wa wachezaji.
 • “Hii ilinifungulia njia nyingine kwa hivyo baada ya kustaafu nimeingilia usimamizi wa michezo. Hata katika Shirikisho la Raga Kenya (KRU) mimi nakaa katika bodi kama mkurugenzi wa raga ya wachezaji saba kila upande,” aliongeza.
 • Kayange pia ni mwenyekiti wa kamati ya kiufundi katika Akademia ya Michezo ya Kenya (KAS).
 • Ni mwakilishi wa wachezaji katika Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC).
 • Pia anahudumu katika Baraza la Wachezaji kwenye Shirika la Kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli duniani (WADA).
 • Kayange ni Mkenya wa kwanza kujumuishwa katika orodha ya mashujaa wa raga duniani. Alitiwa katika orodha hiyo mwaka 2021.
 • Aliwahi kujumuishwa katika orodha ya wawaniaji wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Shirikisho la Raga Duniani mwaka 2009 na 2013.
 • Tags

You can share this post!

Seneta Sifuna amkashifu ‘Mtoto Wa Maumau’...

Ugaidi: Fahamu kwa nini ni ‘makosa’ kuzaliwa...

T L