• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
KCB yajiondoa kwenye mashindano ya Bara Afrika ya voliboli ya wanawake

KCB yajiondoa kwenye mashindano ya Bara Afrika ya voliboli ya wanawake

Na GEOFFREY ANENE

MALKIA wa voliboli barani Afrika mwaka 2006 KCB wamejiondoa kwenye mashindano ya Afrika mwaka 2021 yanayoratibiwa kufanyika Aprili 19 hadi Mei 1 mjini Sousse, Tunisia.

Wanabenki hao wametangaza hayo Alhamisi na kuongeza kuwa wameachilia wachezaji wao wanane waliokuwa wakijiandaa kwa mashindano hayo ya klabu kujiunga na timu ya taifa maarufu kama Malkia Strikers inayojiandaa kwa michezo ya Olimpiki.

“Wachezaji wanane pamoja na makocha wetu wawili wako katika timu ya taifa kwa hivyo KCB haitashiriki makala ya mwaka huu ya mashindano ya klabu za Afrika,” taarifa kutoka KCB ilisema Alhamisi.

Wachezaji wa KCB katika timu ya taifa ni nahodha wa klabu Noel Murambi, nahodha wa Malkia Strikers Mercy Moim pamoja na Edith Mukuvilani, Sharon Chepchumba, Jemima Siangu, Violet Makuto, Leonida Kasaya na Emmaculate Misoki.

Afisa wa kiufundi wa timu ya KCB Paul Bitok ndiye kocha mkuu wa Malkia Strikers naye kocha mkuu wa KCB Japheth Munala ni mmoja wa manaibu wa kocha wa timu ya taifa.

Malkia Strikers ni wawakilishi wa Bara Afrika kwenye Olimpiki mnamo Julai 23 hadi Agosti 8 mwaka huu jijini Tokyo, Japan. Wanarejea kwenye Olimpiki baada ya kukosa makala ya mwaka 2008 (Beijing, Uchina), 2012 (London, Uingereza) na 2016 (Rio de Janeiro, Brazil). Walishiriki Olimpiki mwaka 2000 (Sydney, Australia) na 2004 (Athens, Ugiriki).

Serikali pamoja na Shirikisho la Voliboli Duniani (FIVB), Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K) na Shirikisho la Voliboli Kenya (KVF) wameunda mpangilio mzuri wa kuandaa Malkia Strikers. Timu hiyo itazuru Brazil kwa kambi ya mazoezi ya hali ya juu mwezi Mei, ielekee Bara Ulaya kwa siku 15 na Japan siku 10.

“Tunafurahia kuchangia wachezaji na makocha kwa timu ya taifa kwa hivyo hawatakuwepo kwa majukumu ya klabu hadi Olimpiki zikamilike mjini Tokyo, Japan,” alisema Judith Sidi Odhiambo ambaye ni Mkuu wa Mawasiliano wa KCB.

  • Tags

You can share this post!

Wazee waozea jela sababu ya kesi za unajisi

Olunga kuonyesha waajiri wake wa Al Duhail kuwa anaweza