• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:44 AM
Kevin de Bruyne ajumuika na wenzake kambini mwa Ubelgiji baada ya kufanyiwa upasuaji

Kevin de Bruyne ajumuika na wenzake kambini mwa Ubelgiji baada ya kufanyiwa upasuaji

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

KIUNGO matata wa Manchester City, Kevin de Bruyne, ameungana na wachezaji wenzake kambini mwa Ubelgiji baada ya kufanyiwa upasuaji.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 alivunjika pua na kupata jeraha kwenye jicho la kushoto baada ya kugongana na beki Antonio Rudiger alipokuwa akiwajibikia waajiri wake dhidi ya Chelsea kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Mei 29, 2021 jijini Porto, Ureno.

Ubelgiji wameratibiwa kufungua kampeni zao za Euro dhidi ya Urusi mnamo Juni 12 kabla ya kumenyana na Denmark mnamo Juni 17 kisha Finland mnamo Juni 21. “Upasuaji huo ulikamilika baada ya dakika 20 pekee na ilikuwa sawa kabisa,” akasema kocha wa timu ya taifa ya Ubelgiji, Roberto Martinez.

Ubelgiji kwa sasa wanashikilia nafasi ya kwanza kwenye orodha ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na De Bruyne anatazamiwa kuwa sehemu muhimu kwenye kampeni za kikosi hicho kinachowania taji la kwanza la haiba kubwa kwenye historia ya soka.

“Ilikuwa vyema kwa tatizo la De Bruyne kushughulikiwa mapema. Sasa hatahitaji muda mrefu wa kusalia nje kupona. Madaktari wameridhishwa na hali yake na ameingia kambini,” akasema Martinez.

Jumla ya masogora tisa wanaotandaza soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wamejumuishwa katika kikosi cha wachezaji 26 watakaotegemewa na Ubelgiji kwenye fainali za Euro.

Mbali na De Bruyne pamoja na masogora watatu wa Leicester City – Timothy Castagne, Dennis Praet na Youri Tielemans, kikosi hicho kinajivunia pia maarifa ya fowadi mahiri wa Inter Milan, Romelu Lukaku, na kiungo mzoefu wa Real Madrid, Eden Hazard.

Wachezaji wengine wanaochezea vikosi mbalimbali vya EPL ambao wako kambini mwa Ubelgiji ni beki Toby Alderweireld wa Tottenham Hotspur, fowadi Leandro Trossard wa Brighton, mshambuliaji Christian Benteke wa Crystal Palace na Michy Batshuayi aliyehudumu Palace kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka Chelsea muhula huu wa 2020-21.

Licha ya kufanyiwa upasuaji wa misuli ya miguu mnamo Januari mwaka huu, kiungo matata wa Borussia Dortmund, Axel Witsel, pia yuko katika kikosi cha Ubelgiji na atatarajiwa kujaza nafasi ya nyota wa zamani wa Everton na Manchester United, Marouane Fellaini anayepiga soka ya kulipwa nchini China.

  • Tags

You can share this post!

Mwanariadha mkimbizi Mkongo aliyekimbia kutoka Nairobi hadi...

Chipu wakamilisha kambi ya mazoezi ya Kombe la Afrika