• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Kikao kuandaliwa Disemba 20 kujadili mustakabali wa EPL baada ya maambukizi ya corona kuongezeka

Kikao kuandaliwa Disemba 20 kujadili mustakabali wa EPL baada ya maambukizi ya corona kuongezeka

Na MASHIRIKA

KLABU za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) zitakutana Jumatatu ya Disemba 20, 2021 kujadili hali ya kipute hicho wakati huu ambapo ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya corona linashuhudiwa.

Huku mechi tisa zikiwa tayari zimeahirishwa chini ya kipindi cha wiki moja iliyopita zikiwemo tano kati ya 10 zilizokuwa zisakatwe wikendi hii, vikosi vinataka nafasi ya kuzamia baadhi ya mambo na kuafikiana kuhusu mkondo wa kufuata.

Makocha na manahodha wa klabu mbalimbali za EPL wanatarajiwa pia kuandaa vikao vyao tofauti na kupata mwafaka.

Kocha Steven Gerrard wa Aston Villa amesema anatarajia kwamba mikutano hiyo itatoa “mwanga” kuhusu “malalamishi na maswali mengi ambayo hayajajibiwa”.

Wakati uo huo, kinara wa EPL, Richard Masters, ameandikia vikosi vyote vya kipute hicho kuhimiza wachezaji kupokea chanjo dhidi ya corona huku akisisitiza haja ya kampeni za EPL msimu huu kukamilika.

Kwa upande wake, kocha Thomas Frank wa Brentford ametaka mechi zote zilizopangwa hadi Disemba 26, 2021 kuahirishwa ili kutoa fursa kwa maafikiano mapya.

Japo baadhi wanahisi kwamba likizo ya Krismasi na Mwaka Mpya inastahili kuwa ndefu, wengine akiwemo kocha Jurgen Klopp wa Liverpool anapinga kabisa hata kuwepo kwa likizo hiyo.

Mnamo Disemba 16, 2021, usimamizi wa EPL ulihimiza klabu kuendelea kucheza baadhi ya mechi mradi iwe ni salama kufanya hivyo.

Wakati uo huo, kocha Pep Guardiola amekubaliwa kurejelea maandalizi ya kuongoza kikosi chake kuongoza Manchester City kuvaana na Newcastle United ugenini mnamo Disemba 19, 2021.

“Wasimamizi wa EPL watafanya maamuzi kuhusu iwapo mechi itachezwa au la. Hata hivyo, sote tutahitaji kujua sababu za kila maamuzi yanayofanywa,” akatanguliza kocha wa Arsenal, Mikel Arteta.

“Tulipoanza msimu, tulifahamu kuhusu kuwepo kwa Covid-19 na athari zake. Nina hakika lazima pana mipango mbadala na tutahitaji uwazi,” akaongeza kocha huyo raia wa Uhispania.

Zaidi ya kujadili iwapo mechi zilizosalia zinastahili kuahirishwa, kikao cha Jumatatu kitazamia pia jinsi ambavyo michuano ambayo tayari imeahirishwa itakakavyoratibiwa upya.

Aidha, kuna vuta nikuvute kuhusu iwapo klabu za EPL zitakuwa radhi kuachilia wachezaji kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Afrika (AFCON) na mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022.

Kutolewa kwa droo na ratiba ya mechi za Uefa Nations League mnamo Ijumaa ilifichua jinsi mechi zilivyorundikana kwenye kalenda ya mwaka huu wa 2021-22. Uingereza wamepangiwa kuvaana na Hungary mnamo Juni 4, wiki moja baada ya fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Mei 28, ambayo ni wiki moja pekee baada ya raundi ya mwisho ya EPL kutandazwa Mei 22, 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Lewandowski avunja rekodi nyingine ya ufungaji mabao...

Oparanya aikashifu Jubilee kuhusu kufeli kwa nguzo zake za...

T L