• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Oparanya aikashifu Jubilee kuhusu kufeli kwa nguzo zake za utawala

Oparanya aikashifu Jubilee kuhusu kufeli kwa nguzo zake za utawala

Na SHABAN MAKOKHA

GAVANA wa Kakamega, Wycliffe Oparanya amekashifu utawala wa Jubilee kutokana na kuporomoka kwa utekelezaji wa Nguzo Nne za serikali, akisema kutohusishwa kwa magavana kumechangia hali hiyo.

Bw Oparanya, ambaye ni mwandani wa Kinara wa ODM Raila Odinga, alisema utawala wa Rais Uhuru Kenyatta ulikosa kuhakikisha kuwa kuna ushirikiano kati yake na serikali za kaunti ili kufanikisha nguzo hizo.

Alisisitiza kuwa serikali ya kitaifa ilianzisha sera mbovu na kuwapuuza washikadau muhimu ambao ni wataalamu ambao wangesaidia katika kufanikisha nguzo hizo, ambazo ni kuhakikisha taifa linajitosheleza kwa chakula, makazi ya bei nafuu, utengenezaji wa bidhaa na huduma za afya kwa gharama nafuu.

“Hii nchi ina sera mbovu ambazo zimesababisha utekelezaji wa nguzo hizo ufeli. Inasikitisha kuwa kwa muda ambao umesalia, malengo yake mengi huenda hayataafikiwa,” akasema Bw Oparanya.

Akizungumza mjini Kakamega, Bw Oparanya alitaja sera mbovu kwenye sekta ya afya ambazo zimelazimu kaunti kununua dawa kutoka kwa KEMSA kama kikwazo katika kuafikia usawa katika utoaji wa huduma za afya.

“Kemsa imekuwa ikichelewa kuwasilisha dawa kwa kaunti zetu na hata ikiziwasilisha mara nyingi ni nusu ya kiasi ambacho kiliagizwa. Kemsa haina uwezo wa kuhudumia kaunti zote,” akasema Bw Oparanya.

Mara nyingi kaunti huhitajika kutoa malipo yao mwanzo ndipo ziwasilishiwe dawa, jambo ambalo Bw Oparanya alisema linaenda kinyume na mwongozo wa utendakazi wao kwa mujibu wa sheria za ugatuzi.

Kauli ya Bw Oparanya inakuja siku chache baada ya Naibu Rais William Ruto kulaumu ‘handisheki’ kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga kama iliyochangia kutofanikiwa kwa mpango wao mwanzoni wa kutekeleza ajenda nne kuu za maendeleo.

Dkt Ruto alisema ushirikiano kati ya Rais na Bw Odinga ulizaa Mpango wa Maridhiano (BBI) ambao ulizingatiwa sana na maafisa wa serikali, kuliko nguzo nne za utawala wa Jubilee.

“Nitafufua na kutekeleza ajenda nne ambazo zilikuwa nguzo za utawala wetu. Kufanikiwa kwa mpango huu kulitarajiwa kungesaidia katika kubuni nafasi za ajira kwa vijana na kuimarisha maendeleo ya kaunti,” akasema Dkt Ruto.

You can share this post!

Kikao kuandaliwa Disemba 20 kujadili mustakabali wa EPL...

Magoha asisitiza KCPE, KCSE ni Machi 2022

T L