• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 7:53 PM
Kilio Man-U, Arsenal ikipiga sherehe Uefa

Kilio Man-U, Arsenal ikipiga sherehe Uefa

MUNICH, Ujerumani

Kipa Andre Onana ameamua kubeba msalaba kwa matokeo duni ya Manchester United baada ya kulimwa 4-3 na Bayern Munich kwenye Klabu Bingwa Ulaya mnamo Jumatano katika siku ambayo Arsenal ilipata raha tele kulipua PSV Eindhoven 4-0.

Casemiro alifunga mabao mawili naye Rasmus Hojlund goli moja mashetani wekundu wa United wakizamishwa na Bayern kupitia kwa mabao ya Leroy Sane, Serge Gnabry, Harry Kane (penalti) na Matthys Tel katika Kundi A ugani Allianz Arena.

Wanabunduki wa Arsenal walirejea kwa kishindo kwenye Klabu Bingwa Ulaya baada ya miaka sita kwa kumiminia PSV mabao kupitia kwa Bukayo Saka, Leandro Trossard, Gabriel Jesus na Martin Odegaard katika Kundi B ugani Emirates.

United imefungwa mabao 14 katika mechi sita. Onana,27, aliomba kuhojiwa baada ya United kupoteza dhidi ya Bayern na akakubali kosa lilikuwa lake.

“Hali ni ngumu. Tulianza vyema na, baada ya kosa langu, tukapoteza mwelekeo wa mechi. Ni hali ngumu kwangu kwa sababu nilisababishia timu masaibu. Ni kwa sababu yangu hatukushinda mchuano huu,” alisema raia huyo wa Cameroon na kutaka wasahau yaliyopita na kuganga yajayo.

“Ni maisha ya kipa. Bayern hawakuwa wamepata nafasi yoyote. Nilifanya kosa waliponisukumia kombora la kwanza na tukafungwa. Tulipigana hadi kipenga cha mwisho, lakini natambua kuwa hatukushinda kwa sababu yangu. Nina mengi ya kudhihirishia mashabiki wa United. Sijakuwa na mwanzo mzuri nilivyotaka,” aliongeza Onana aliyenunuliwa kwa Sh8.5 bilioni kutoka Inter Milan.

Kocha Erik ten Hag ameapa kusaidia sajili huyo mpya kutulia akionekana kulaumu timu nzima kwa kutokuwa katika kiwango kimoja kutafuta matokeo mazuri.

United sasa imepoteza kwa mara ya nne katika mechi sita msimu huu. Ni mara ya kwanza ilikubali nyavu zake kuchanwa mara nne katika mechi moja ya Klabu Bingwa Ulaya tangu mwaka 1994 ilipopoteza 4-0 mikononi mwa Barcelona.

Kocha wa Bayern, Thomas Tuchel alikiri kuwa vijana wake walibahatika kumaliza mechi hiyo kwa ushindi.

Odegaard aling’ara dhidi ya PSV. Mtihani mkali wa Arsenal waja kwenye Ligi Kuu dhidi ya majirani Tottenham Hotspur hapo Septemba 24.

Matokeo (Septemba 20):

Real Madrid 1 Union Berlin 0, Galatasaray 2 Copenhagen 2, Bayern Munich 4 Manchester United 3, Benfica 0 Salzburg 2, Braga 1 Napoli 2, Arsenal 4 PSV Eindhoven 0, Sevilla 1 Lens 1, Real Sociedad 1 Inter Milan 1

  • Tags

You can share this post!

Polisi wasaka mwanamke mshukiwa wa mauaji aliyenaswa...

Kioni ataka mazungumzo baina ya Kenya Kwanza na Azimio...

T L