• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Kocha Ryan Mason aaminiwa nafasi ya kushikilia mikoba ya Spurs hadi mwisho wa msimu huu

Kocha Ryan Mason aaminiwa nafasi ya kushikilia mikoba ya Spurs hadi mwisho wa msimu huu

Na MASHIRIKA

KOCHA Ryan Mason, 29, amesema ni “fahari na tija tele” kwamba ameaminiwa fursa ya kuwa kocha mshikilizi wa Tottenham Hotspur hadi mwishoni mwa msimu huu baada ya kutimuliwa kwa mkufunzi Jose Mourinho.

Mason ambaye ni kiungo wa zamani wa Spurs, alistaafu kwenye ulingo wa usogora mnamo 2018 baada ya kupata jeraha la fuvu na amekuwa akiwanoa chipukizi wa akademia ya kikosi hicho.

Aliongoza vipindi viwili vya mazoezi ya kikosi chake mnamo Jumanne, siku moja baada ya Mourinho ambaye ni raia wa Ureno kupigwa kalamu baada ya miezi 17.

Tottenham wanatarajiwa leo kualika Southampton kwa minajili ya mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kabla ya kushuka dimbani kuvaana na Manchester City kwenye fainali ya Carabao itakayowakutanisha ugani Wembley, Uingereza mnamo Aprili 25, 2021.

Chris Powell na Nigel Gibbs watakuwa wasaidizi wa kocha Mason kwa muda chini ya Ledley King ambaye atakuwa msaidizi mkuu wa Mason katika majukumu ya kunoa kikosi cha kwanza. Michel Vorm ameteuliwa kuwa kocha wa makipa kambini mwa Tottenham.

Fowadi na nahodha Harry Kane hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Tottenham kwenye fainali ya Carabao Cup. Hii ni baada ya sogora huyo raia wa Uingereza kupata jeraha la mguu katika mchuano uliopita wa EPL uliowakutanisha na Everton. Mechi hiyo iliyokamilika kwa sare ya 2-2 ugani Goodison Park mnamo Aprili 16, 2021 ilikuwa ya mwisho kwa Mourinho kusimamia kambini mwa Tottenham.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

KINA CHA FIKRA: Asilan usikubali kushindwa hata kabla ya...

KAULI YA MATUNDURA: Shabaan Robert na Muyaka walinyanyasa...