• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 8:50 AM
Kocha wa Nakuru City Queens ajiuzulu

Kocha wa Nakuru City Queens ajiuzulu

NA TOTO AREGE

KOCHA mkuu wa Nakuru City Queens Chrispin Wesonga amejiuzulu baada ya kuiongoza klabu hiyo kwa msimu mmoja pekee.

Wesonga aliongoza timu hiyo ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL), kumaliza katika nafasi ya sita kwenye jedwali na pointi 32 msimu jana, alama 23 nyuma ya mabingwa watetezi Vihiga Queens.

“Sielewi kwanini aliondoka ghafla kupitia kundi letu la WhatsApp Jumapili jioni. Napanga kufanya mazungumzo naye ili tuweze kutatua masuala yetu ya ndani,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa klabu Bernard Esitoko.

Akizungumza na Taifa Spoti jana Jumatatu kwa njia ya simu, Wesonga alithibitisha kuondoka kwake kwenye timu hiyo.

“Ifahamike kuwa, nimeondoka klabuni tena na huu ni uamuzi nilioufanya mwenyewe. Tangia niwasili kwenye timu, timu hiyo haijakuwa ikiendeshwa kwa ustaarabu. Uongozi wa klabu hiyo uliniomba kuwasaidia mwanzoni mwa msimu jana na ni kazi ambayo nilifanya bila malipo yoyote,” alisema Wesonga.

“Nilisimamia klabu peke yangu hata bila msaidizi. Tulikuwa na msimu mbaya sana na licha ya changamoto zote, wasichana walipigania klabu. Nawatakia kila la heri msimu ujao,” aliongeza Wesonga, aliyekuwa kocha wa zamani wa Nakuru All Stars, Chuo Kikuu cha Egerton na Nakuru Bucks FC.

Kocha huyo mwenye Leseni ya CAF D 2023, pia aliongoza Nakuru kumaliza wa pili katika mashindano ya Kombe la Wanawake la Shirikisho la Soka la nchini (FKF) mnamo Juni 4, 2023 ambapo walipoteza 4-1 dhidi ya Ulinzi Starlets katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi.

Nakuru walitunukiwa Sh250,00 huku Ulinzi wakirudi nyumbani na Sh500,000 kama mabingwa.

Taifa Spoti inaweza kuripoti kuwa, Wesonga, pamoja na wachezaji wakongwe na chipukizi walipokea tu Sh3,500, Sh3,000 na Sh10,000 mtawalia kutokana na pesa walizotuzwa.

Wachezaji hao sasa wamegoma kufanya mazoezi ya kujiandaa kwa ajili ya msimu mpya.

“Afadhali kuacha soka kwa sababu sisi wachezaji tunapigania timu na mwisho wa yote tunapata hela kidogo. Tunastahili zaidi ikizingatiwa tuna familia ambazo zinatutegemea na kama klabu haiwezi kuwatunza wachezaji wake. Basi tutaondoka,” alisema mmoja wa wachezaji ambaye hakutaka kutajwa jina.

  • Tags

You can share this post!

Serikali, Hand in Hand washikana mikono kusafisha...

Mzungu atupwa jela miaka 81 kwa kuwadhulumu kingono...

T L