• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 11:29 AM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Canada waaga kipute katika hatua ya makundi baada ya kutandikwa na Croatia

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Canada waaga kipute katika hatua ya makundi baada ya kutandikwa na Croatia

Na MASHIRIKA

CROATIA walizima matumaini ya Canada kuingia hatua ya 16-bora kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka huu baada ya kutoka nyuma na kupepeta Canada 4-1 katika pambano la Kundi F ugani Khalifa International mnamo Jumapili.

Alphonso Davies aliwaweka Canada kifua mbele katika dakika ya pili baada ya kushirikiana vilivyo na Tajon Buchanan.

Hata hivyo, Croatia waliotinga fainali ya 2018 nchini Urusi hawakufa moyo. Walijituma na kukita kambi langoni mwa Canada na wakafaulu kucheka na nyavu kupitia kwa Andrej Kramaric aliyekamilisha krosi ya Ivan Perisic. Marko Livaja aliwaweka Croatia kifua mbele katika dakika ya 44 kabla ya Kramaric na Lovro Majer kufunga mabao mengine katika kipindi cha pili.

Canada bado hawana alama yoyote kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka huu na sasa wameaga kipute hicho katika hatua ya makundi. Fainali za mwaka huu zilikuwa za kwanza kwa kikosi hicho kunogesha tangu mwaka wa 1986. Sasa watafunga kampeni zao za Kundi F dhidi ya Morocco mnamo Disemba 1, 2022 huku Croatia ambao wamepoteza mechi moja pekee kati ya 18 zilizopita, wakivaana na Ubelgiji.

Kufikia sasa, Croatia wanaselelea kileleni mwa Kundi F kwa alama nne sawa na Morocco waliokomoa Ubelgiji 2-0 katika mchuano mwingine wa Jumapili. Ubelgiji waliofungua kampeni zao kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Canada wana alama tatu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ujerumani na Uhispania nguvu sawa...

ZARAA: Mfumo ulioboreshwa kuendeleza kilimo mijini

T L