• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Liverpool waponda Leeds United na kuendeleza presha kwa Man-City kileleni mwa jedwali la EPL

Liverpool waponda Leeds United na kuendeleza presha kwa Man-City kileleni mwa jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL walipunguza zaidi pengo la alama kati yao na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Manchester City baada ya kuponda Leeds United 6-0 mnamo Jumatano usiku ugani Anfield.

Ushindi huo ulikuwa wa sita mfululizo kwa Liverpool ya kocha Jurgen Klopp kusajili katika soka ya EPL. Sasa wanakamata nafasi ya pili kwa alama 60, tatu pekee nyuma ya viongozi Man-City ambao pia wametandaza jumla ya mechi 26.

Matokeo hayo ya Liverpool dhidi ya Leeds yanatarajiwa sasa kuwapa motisha zaidi ya kuzamisha Chelsea kwenye fainali ya Carabao Cup itakayowakutanisha ugani Wembley mnamo Februari 27, 2022. Chelsea watashuka dimbani kwa ajili ya fainali hiyo wakilenga pia kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 2-0 dhidi ya Lille katika mchuano wao uliopita kwenye gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ugani Stamford Bridge.

Liverpool walianza mechi yao dhidi ya Leeds kwa matao ya juu na wakafunga mabao matatu chini ya dakika 20 za kwanza za mchezo.

Mawili kati ya mabao hayo yalitokana na penalti mbili zilizofungwa na Mohamed Salah ambaye pia alichangia bao la Joel Matip aliyefungia Liverpool kwa mara ya kwanza tangu Disemba 2020.

Mabao mengine ya Liverpool yalifumwa kimiani kupitia kwa beki Virgil van Dijk na fowadi Sadio Mane aliyecheka na nyavu mara mbili.

Liverpool kwa sasa wanajivunia tofauti kubwa ya mabao (50) kuliko 46 inayojivuniwa na washindani wao wakuu Man-City ambao watamenyana nao mnamo April 9, 2022 ugani Etihad.

“Pengo linalotutenganisha na Man-City ni dogo. Sasa tuna ulazima wa kushinda mechi zetu zote 12 zilizosalia kwa idadi kubwa ya mabao. Hiyo ndiyo njia ya pekee kwa Liverpool kutawazwa wafalme wa EPL muhula huu,” akasema Klopp.

Man-City wanaonolewa na mkufunzi Pep Guardiola walikuwa wakijivunia pengo la alama 14 kati yao na Liverpool baada ya kutandika Chelsea mnamo Januari 15, 2022. Kufikia wakati huo, Man-City walikuwa tayari wametandaza mechi mbili zaidi kuliko Liverpool.

Liverpool kwa sasa wamefunga mabao 70, mawili zaidi kuliko idadi ya mabao ambayo walitia kapuni kutokana na mechi 38 walipoambulia nafasi ya tatu mnamo 2020-21. Kati ya magoli hayo 70 ligini, Salah anajivunia 19.

Chini ya kocha Marcelo Bielsa, Leeds sasa wanajivunia alama 23 na wako katika hatari ya kuteremshwa ngazi kwenye EPL muhula huu iwapo watashindwa kuhimili presha kutoka kwa Everton, Newcastle United na Burnley. Watford na Norwich wanashikilia nafasi mbili za mwisho jedwalini kwa alama 18 na 17 mtawalia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Man-United walazimishia Atletico Madrid sare katika mkondo...

Burnley wazidisha masaibu ya kocha Antonio Conte kambini...

T L