• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 3:25 PM
Lukaku alivyofufua makali yake nchini Italia na kusaidia Inter kutwaa taji la kwanza la Serie A baada ya miaka 11

Lukaku alivyofufua makali yake nchini Italia na kusaidia Inter kutwaa taji la kwanza la Serie A baada ya miaka 11

Na MASHIRIKA

INTER Milan walijizolea taji la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) msimu huu kwa mara ya kwanza tangu 2009-10.

Miongoni mwa wanasoka waliochangia ufanisi wa kikosi hicho cha kocha Antonio Conte ni fowadi wa zamani wa Manchester United, Romelu Lukaku.

Sogora huyo raia wa Ubelgiji aliposajiliwa na Inter kwa Sh10.3 bilioni mnamo Agosti 2019, alikuwa na kibarua kizito cha kujaza pengo la Mauro Icardi – raia wa Argentina aliyekuwa mshambuliaji tegemeo wa kikosi hicho.

Ingawa kampeni za Icardi ambaye kwa sasa anavalia jezi za Paris Saint-Germain (PSG) zilikuwa na panda-shuka tele kutokana na majeraha, alikuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo zaidi huku akipachika wavuni jumla ya mabao 11 kutokana na mechi 169 za Serie A.

Ingawa hivyo, makali yake yalididimia kadri muda ulivyopita na asilimia 26 ya mabao hayo aliyofungia Man-United yalitokana na mechi alizozipiga katika miezi miwili ya kwanza ya kuhudumu kwake uwanjani Old Trafford.

Lukaku aliondoka Man-United akijivunia kufungia miamba hao wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) jumla ya mabao 42 kutokana na mechi 96 chini ya kipindi cha miaka miwili.

Hata hivyo, makali ya Lukaku, 27, yalifufuka pakubwa alipotua kambini mwa Inter ambao chini ya Conte, wamefaulu hatimaye kukomesha ukiritimba wa Juventus waliokuwa wkaiwania taji la Serie A kwa mara ya 10 mfululizo msimu huu wa 2020-21.

Inter walikamilisha kampeni za 2018-19 katika nafasi ya nne jedwalini huku pengo la alama 21 likitamalaki kati yao na Juventus waliotwaa ubingwa baada ya kujizolea alama 90.

Katika msimu wake wa kwanza kambini mwa Inter, Conte aliongoza waajiri wake kuambulia nafasi ya pili kwa alama 82, moja pekee nyuma ya Juventus waliokuwa chini ya mkufunzi wa zamani wa Napoli na Chelsea, Maurizio Sarri.

Akiwa Everton na Man-United, Lukaku alikuwa akichezeshwa mara kwa mara peke yake kama mvamizi mkuu. Lakini alipata mshambuliaji mwenza kambini mwa Inter, Lautaro Martinez, ambaye amekuwa akishirikiana naye pakubwa katika mfumo wa 3-5-2 unaopendelewa sana na Conte.

Mbali na kuundiana nafasi za kufunga, wawili hao wamekuwa wakitikisa nyavu za wapinzani kwa wepesi huku kila mmoja akichangia mabao 18 kutokana na mechi 64 zilizopita ambazo zimewashuhudia wakifunga magoli 87 kwa pamoja katika mashindano yote.

Hakuna mchezaji mwingine yeyote wa Serie A ambaye amechangia idadi kubwa zaidi ya mabao kuliko Lukaku ambaye amechangia magoli 10 ligini kufikia sasa msimu huu.

Kati ya mabao 21 ambayo amefungia Inter kufikia sasa ligini, manane yamekuwa dhidi ya AC Milan, Atalanta, Juventus, Napoli, Lazio na AS Roma ambao ni wapinzani wao wakuu katika Ligi Kuu ya Italia. Lukaku anashikilia nafasi ya pili nyuma ya Cristiano Ronaldo wa Juventus (mabao 27) kwenye orodha ya wafungaji bora wa Serie A kufikia sasa msimu huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Jaji Mkuu afaa kuteuliwa apokezwe mikoba ndipo mtangulizi...

SHINA LA UHAI: Mto Ewaso Ng’iro hatarini kukauka