• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 8:50 AM
Jaji Mkuu afaa kuteuliwa apokezwe mikoba ndipo mtangulizi wake aondoke rasmi, apendekeza Cherargei

Jaji Mkuu afaa kuteuliwa apokezwe mikoba ndipo mtangulizi wake aondoke rasmi, apendekeza Cherargei

Na SAMMY WAWERU

SENETA wa Kaunti ya Nandi Samson Cherargei amependekeza asasi huru serikalini kama idara ya mahakama, ziwe zinateua viongozi wake kabla ya wanaostaafu kuondoka rasmi afisini.

Bw Cherargei amesema hatua hiyo itawezesha wanoingia afisini kutwaa uongozi kwa namna inayofaa ili kuendeleza utendakazi wa watangulizi wao bila kutatizika.

Akitumia mfano wa Mahakama ya Juu zaidi nchini, seneta huyo alisema mchakato wa kuteua Jaji Mkuu umechukua muda mrefu suala ambalo anasema linalemaza utendakazi wa idara ya mahakama.

Cherargei alisema hayo baada ya jopokazi la makamishna wa tume ya huduma za mahakama (JSC) kutangaza kumteua Bi Martha Koome kama Jaji Mkuu.

Majuma kadha yaliyopita, JSC iliendesha mchakato wa kupiga msasa wawaniaji wa wadhifa huo uliosalia wazi baada ya Jaji Mkuu David Maraga kustaafu rasmi Januari 12, 2021.

“Taasisi huru za kiserikali kama vile idara ya mahakama, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), idara ya polisi, kati ya nyinginezo zinapaswa kuteua viongozi wake kabla walioko kuondoka ili kuwapa jukwaa bora wanaotwaa uongozi kuendeleza utendakazi,” akasema seneta Cherargei, akilalamikia kukawia kuteuliwa kwa mrithi wa Maraga.

Rais Uhuru Kenyatta alipokezwa jina la Jaji Mkuu mteule Martha Koome ambaye atapigwa msasa na bunge kabla ama kukataliwa au kuidhinishwa rasmi na aapishwe.

Jopokazi la JSC Jumatatu lilianza mchakato wa kutafuta majaji wa mahakama ya juu zaidi nchini, ambao watakuwa chini ya Jaji Mkuu.

You can share this post!

Valencia wamtimua kocha Javi Gracia baada ya matokeo duni...

Lukaku alivyofufua makali yake nchini Italia na kusaidia...