• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Man-City na Liverpool bado unyo kwa unyo katika EPL baada ya kuambulia sare ya 2-2 ugani Etihad

Man-City na Liverpool bado unyo kwa unyo katika EPL baada ya kuambulia sare ya 2-2 ugani Etihad

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walidumisha pengo la alama moja kati yao na Liverpool kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kulazimishiwa sare ya 2-2 na masogora hao wa kocha Jurgen Klopp mnamo Jumapili ugani Etihad.

Zikisalia mechi saba pekee kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kampeni za EPL msimu huu kutamatika rasmi, Man-City wanaonolewa na kocha Pep Guardiola wanadhibiti kilele cha jedwali la EPL kwa pointi 73.

Wakichezea katika uwanja wao wa nyumbani, Man-City waliwekwa kifua mbele na Kevin de Bruyne katika dakika ya tano kabla ya Diogo Jota kusawazisha mambo baada ya kushirikiana vilivyo na Trent Alexander-Arnold dakika nane baadaye. Bao la Jota lilikuwa lake la 15 katika EPL akivalia jezi za Liverpool msimu huu.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City walitamalaki mchezo katika kipindi cha kwanza huku Gabriel Jesus akimzidi maarifa beki Alexander-Arnold na kupachika wavuni bao la pili la Man-City kutokana na krosi ya Joao Cancelo kunako dakika ya 36.

Hata hivyo, Sadio Mane aliyekuwa akiadhimisha miaka 30 ya kuzaliwa kwake aliwarejesha Liverpool mchezoni katika dakika ya 47 baada ya kujaza kimiani krosi ya Mohamed Salah.

Bao la Raheem Sterling wa Man-City lilikataliwa na refa katika dakika ya 76 baada ya kubainika kwamba sogora huyo alitikisa nyavu za waajiri wake wa zamani akiwa ameotea. Riyad Mahrez naye aliyeletwa uwanjani katika kipindi cha pili alipoteza nafasi kadhaa za wazi za kufungia Man-City bao la ushindi sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Liverpool walishuka dimbani wakijivunia rekodi ya kushinda mechi 10 mfululizo ligini na nane za ugenini katika mashindano yote.

Liverpool sasa wameshinda mara 22, kutoka sare mara saba na kupoteza michuano miwili. Tofauti na Man-City ambao wamefunga mabao 72 na kuruhusu wapinzani kutikisa nyavu zao mara 20 ligini, Liverpool wamepachika wavuni magoli 79 na kuokota mpira kimiani mara 22.

Sawa na Man-City waliokomoa Atletico Madrid 1-0 katika mkondo wa kwanza wa robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Aprili 5, 2022 Liverpool nao walijibwaga ugani wakilenga kuendeleza ubabe uliowazolea ushindi wa 3-1 dhidi ya Benfica nchini Ureno.

Man-City walifungua mwaka wakijivunia pengo la alama nane kati yao na Liverpool, kila mmoja akiwa ametandaza mechi 21 ligini. Hata hivyo, sare dhidi ya Southampton (1-1) na Crystal Palace (0-0) pamoja na kichapo cha 3-2 kutoka kwa Tottenham Hotspur kati ya Januari na Machi ni matokeo yaliyopoteza dira ya Man-City wanaofukuzia taji la sita la EPL na la nne chini ya Guardiola.

Man-City sasa wanajiandaa kurudiana na Atletico kwenye UEFA mnamo Aprili 13, 2022 nchini Uhispania kabla ya kuvaana tena na Liverpool siku tatu baadaye kwenye nusu-fainali ya Kombe la FA ugani Wembley.

Man-City waliokomoa Burnley 2-0 katika mechi yao iliyopita ligini, hawajapoteza pambano lolote kati ya manane yaliyopita katika mashindano yote. Tangu Palace iwatandike 2-0 mnamo Oktoba 2021, Man-City ambao wamepachika wavuni mabao 42 katika mechi za EPL ugani Etihad msimu huu, hawajawahi kukamilisha mchuano wowote wa ligi bila kufunga bao katika uwanja wao wa nyumbani.

Baada ya kulemea Chelsea kwa penalti 11-10 na kunyanyua ubingwa wa Carabao Cup mwishoni mwa Februari, Liverpool wangali na ndoto za kujizolea mataji matatu zaidi msimu huu – EPL, UEFA na Kombe la FA.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool wameshinda mechi 17 kati ya 19 zilizopita katika mashindano yote. Inter Milan ya Italia ndiyo timu ya pekee iliyobwaga wapambe hao 1-0 katika mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora ya UEFA mnamo Machi 18, 2022 uwanjani Anfield.

Kati ya mechi 187 zilizopita kati ya Liverpool na Man-City, masogora wa Klopp wameshinda mara 88 na kuambulia sare mara 51 huku Man-City ikiwatandika mara 48. Timu hizo zilitoshana nguvu kwa sare ya 2-2 zilipokutana tena katika mkondo wa kwanza wa EPL ugani Anfield mnamo Oktoba 2021.

MATOKEO YA EPL (Jumapili):

Brentford 2-0 West Ham

Leicester 2-1 Crystal Palace

Norwich City 2-0 Burnley

Man-City 2-2 Liverpool

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

MAPISHI KIKWETU: Kuandaa viazi na samaki mbichi

Kenya Open ya kulenga shabaha kwa bastola yavutia nchi 10

T L