• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Man-City sasa katika hatari ya kupitwa na Liverpool ligini baada ya kulazimishiwa sare tasa na Palace

Man-City sasa katika hatari ya kupitwa na Liverpool ligini baada ya kulazimishiwa sare tasa na Palace

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walipoteza fursa ya kufungua pengo la alama sita kati yao na nambari mbili Liverpool kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumatatu usiku baada ya kulazimishiwa sare tasa na Crystal Palace ugani Selhurst Park.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City walitamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira huku beki Aymeric Laporte akishuhudia makombora yake mawili yakibusu mwamba wa lango la Palace wanaotiwa makali na mkufunzi Patrick Vieira.

Ina maana kwamba Liverpool sasa watapunguza pengo la alama kati yao na Man-City hadi alama moja pekee iwapo watawakomoa Arsenal ugani Emirates mnamo Machi 16, 2022.

Licha ya kuhangaisha wageni wao, Palace hawakufanya mashambulizi mengi wala kutatiza kipa wa Man-City.

Alama moja ambayo Palace walijizolea dhidi ya Man-City sasa inawadumisha katika nafasi ya 11 jedwalini kwa alama 34.

Wiki nane zilizopita, Man-City walikuwa wakijivunia pengo la alama 13 kileleni mwa jedwali la EPL huku dalili zote zikiashiria kwamba walikuwa pazuri zaidi kuhifadhi taji la kipute hicho muhula huu wa 2021-22. Hata hivyo, Liverpool waliokuwa wakikamata nafasi ya tatu wakati huo, walikuwa na mechi mbili zaidi za kutandaza ili kufikia idadi ya michuano iliyokuwa imepigwa na Man-City.

Lakini baada ya Man-City kuambulia sare tasa dhidi ya Palace mnamo Jumatatu, sasa pengo la alama kati yao na Liverpool ni pointi nne pekee.

Nafuu zaidi kwa Liverpool ni kwamba wana mechi moja zaidi ya kusakata ili kufikia idadi ya michuano 29 ambayo imetandazwa na Man-City watakaokuwa wenyeji wa Liverpool ugani Etihad mnamo Aprili 10, 2022.

Ilikuwa mara ya pili msimu huu kwa Man-City kukamilisha mechi bila kufunga bao. Mara ya kwanza kwa Man-City kutofunga bao ligini muhula huu ni wakati walipopepetwa 2-0 na Palace mnamo Oktoba 2021 ugani Etihad. Masogora hao wa Guardiola walishuka dimbani dhidi ya Palace wakijivunia rekodi ya kushinda mechi 16 kati ya 18.

Palace kwa sasa hawajashindwa katika mechi yoyote kati ya tano zilizopita na nusura wafunge mabao kupitia kwa Wilfried Zaha, Michael Olise na Conor Gallagher mwanzoni mwa kipindi cha pili. Walijibwaga ugani wakiwa wamejizolea alama moja pekee kutokana na mechi nne za awali katika uwanja wao wa nyumbani mwaka huu wa 2022.

Palace sasa wanajiandaa kwa mechi ya robo-fainali ya Kombe la FA dhidi ya Everton ugani Selhurst Park mnamo Machi 20 huku Man-City wakiwa wageni wa Southampton uwanjani St Mary’s.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wajumbe 5,000 wa UDA kumwidhinisha Ruto leo

Mshukiwa mkuu wa unyama Forest Road akamatwa

T L