• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:01 PM
Man-City wapepeta Sporting Lisbon bila huruma katika UEFA

Man-City wapepeta Sporting Lisbon bila huruma katika UEFA

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City waliweka hai matumaini ya kutinga robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu kirahisi baada ya kuponda Sporting Lisbon ya Ureno 5-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza mnamo Jumanne usiku ugenini.

Bernardo Silva alikuwa miongoni mwa wachezaji wanne wa zamani wa Benfica ya Ureno katika mchuano huo. Walizomewa na mashabiki wa nyumbani kila walipogusa mpira. Hata hivyo, aliwanyamazisha alipofungia Man-City bao la pili na la nne katika gozi hilo.

Mabao mengine ya Man-City wanaopigiwa upatu wa kunyanyua taji la UEFA msimu huu yalijazwa kimiani kupitia kwa Riyad Mahrez, Phil Foden na Raheem Sterling aliyeshirikiana vilivyo na Kevin de Bruyne katika safu ya mbele.

Kichapo hicho ndicho kinono zaidi kuwahi kusajiliwa na kikosi katika mchuano wa UEFA ugenini na kiliwezesha Man-City kufikia rekodi yao ya 2016-17 walipotandika Steaua Bucharest 5-0 katika mchuano wa mchujo wa kufuzu kwa soka ya UEFA.

Mechi ya marudiano kati ya Man-City na Sporting itasakatiwa ugani Etihad, Uingereza mnamo Machi 16, 2022. Sporting walikamilisha kampeni za Kundi C katika nafasi ya pili nyuma ya Ajax ya Uholanzi huku Man-City wakitawala Kundi A kwa pointi 12.

Man-City ambao pia wanawania taji ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Kombe la FA msimu huu, walishuka dimbani wakiwa na motisha ya kupepeta Norwich City 4-0 katika EPL mnamo Februari 12, 2022.

Kufikia sasa, wanaselelea kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 63, tisa zaidi kuliko nambari mbili Liverpool. Watajizolea taji la nne la UEFA chini ya misimu mitano iwapo watatawazwa wafalme muhula huu chini ya kocha Pep Guardiola.

Sporting wananogesha hatua ya 16-bora ya UEFA kwa mara ya kwanza tangu 2008-09 walipokomolewa 12-1 na Bayern Munich ya Ujerumani.

You can share this post!

Man-United wakomoa Brighton na kuingia nne-bora EPL

Wito vijana wa Kiislamu wapewe vitambulisho bila ubaguzi...

T L