• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Mashabiki wa AFC Leopards waruhusiwa kurejea uwanjani

Mashabiki wa AFC Leopards waruhusiwa kurejea uwanjani

NA JOHN ASHIHUNDU

SHIRIKISHO la Soka Nchini (FKF) limeruhusu mashabiki wa AFC Leopards warejee uwanjani kuanzia wikendi hii.

Barua iliyowekwa saini na Afisa Mkuu wa FKF, Barry Otieno ilisema kamati ya kusikiliza kesi za rufaa katika shirikisho hilo ilikutana Alhamisi na kuamua marufuku ya mechi iliyowekewa mashabiki wa klabu hiyo iondolewe ili waanze kurudi uwanjani kushangilia timu yao ambayo kesho Jumapili itakabiliana na Nzoia Sugar FC, ugani Nyayo.

Chini ya mwenyekiti Janet Katisya, kamati hiyo ilisema imesikiza kesi ya kujitetea kutoka kwa klabu hiyo na kuamua kulegeza kamba.Mashabiki wa Leopards walipigwa marufuku kuingia uwanjani baada ya kuhusishwa na fujo zilizotokea uwanjani Bukhungu mnamo Aprili 19 ambapo mwamuzi wa mechi alijeruhiwa.

Mbali na kupigwa marufuku na kupokonywa pointi tatu, klabu hiyo vile vile ilitozwa Sh500,000 kufutia fuzo hizo zilizotokea wakicheza na Kakamega Homeboyz kabla ya mechi hiyo kutibuka dakika 34 Homeboyza wakiongoza kwa 1-0, bao lililofungwa na Hillary Otieno.

Leopards pia iliamrishwa igharimie malipo ya hospitali ya refa Micheal Obuya aliyeumia siku hiyo, lakini usimamizi wa klabu hiyo uliamua kufuata utaratibu kuhakikisha haki imetendeka kwa ajili ya kudumisha heshima ya timu hiyo kongwe.

FKF kadhalika ilipendekeza kocha mkuu wa klabu hiyo, Patrick Aussems na naibu wake Lawrence Webo wafanyiwe uchunguzi baada ya kuvuruga amani siku hiyo.

Tangu ipigwe marufuku mnamo, mashabiki wa Leopards wamekuwa wakilipa ada za kiingilio hata wakiwa majumbani mwao ili kusaidia timu hiyo moja kwa moja, na kukataa kabisa kusafiri kuchangia timu pinzani.

Mashabiki hao walitoa kauli mbiu ya ‘Operation Susia Stadi Jenga Ingwe Mpesa Paybill 522522, Account Number 11778034666’, ambapo wamekuwa wakitoa Sh500,000 na Sh200,000 kusapoti timu yao kifedha na kusubiri matokeo wakiwa majumbani mwao.

Akizungmza kuhusu hatua ya FKF, mwenyekiti wa klabu hiyo, Dan Shikanda alisema timu yake imekuwa ikidhulumiwa bila hatua kuchukuliwa.

Alisema kutibuka kwa mechi mjini Kakamega kulitokana uzembe wa mwamuzi na ukosefu wa askari wa kutosha siku hiyo.

Mashabiki wa AFC Leopards wakiwa katika uwanja wa Bukhungu mjini Kakamega mnamo Aprili 16, 2023 wakati wa mechi ya AFC Leopards dhidi ya Kakamega Homeboyz. PICHA | ISAAC WALE

Mwekahazina wa klabu hiyo, Oliver Napali alisema kwa kutohudhuria mechi nne, klabu hiyo imepoteza zaidi ya Sh3 milioni ambazo wangeokota mlangoni.

Shikanda alieleza masikitiko yake kufuatia uamuzi wa kupiga mashabiki marufuku, huku akisisitiza kwamba timu yake iliwasilisha ushahidi wa kutosha kujitetea kuhusiana na usalama duni na upendeleo wa hadharani kutoka kwa ripoti ya maafisa waliosimamia mechi hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Mfalme Charles III atawazwa rasmi kwenye sherehe babukubwa

Lesiit ateuliwa kuongoza jopo la Shakahola

T L