• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 8:11 PM
Messi afunga mawili akiweka rekodi ya kuchezea Barcelona idadi kubwa zaidi ya mechi

Messi afunga mawili akiweka rekodi ya kuchezea Barcelona idadi kubwa zaidi ya mechi

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi, 33, alisherehekea rekodi ya kufikia jumla ya mechi 768 akichezea Barcelona kwa kupachika wavuni mabao mawili katika ushindi wa 6-1 waliousajili dhidi ya Real Sociedad kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Machi 21, 2021.

Fowadi na nahodha huyo raia wa Argentina alivunja rekodi ya mechi 767 za aliyekuwa kiungo wa miamba hao Xavi Hernandez ambaye kwa sasa anawatia makali wanasoka wa kikosi cha Al-Sadd nchini Qatar.

Ushindi kwa Barcelona uliwapaisha hadi nafasi ya pili kileleni mwa jedwali la La Liga kwa alama 62, nne pekee nyuma ya viongozi wa jedwali Atletico Madrid.

Griezmann aliwafungulia Barcelona ukurasa wa mabao katika dakika ya 37 kabla ya Sergino Dest kufunga mawili kunako dakika za 43 na 53. Fowadi raia wa Ufaransa, Ousmane Dembele pia alifunga goli katika dakika ya 71 baada ya Messi kupachika wavuni goli lake la kwanza katika dakika ya 56 kisha la pili kunako dakika ya 89.

Chini ya kocha Imanol Alguacil, Sociedad walifutiwa machozi na Ander Barrenetxea kunako dakika ya 77 katika uwanja wao wa nyumbani wa Anoeta.

Messi kwa sasa amepachika wavuni jumla ya mabao 23 na kuchangia mengine manane katika kampeni za La Liga msimu huu na ndiye anayeongoza orodha ya wafungaji bora wa kipute hicho.

Messi kwa sasa ndiye mfungaji bora wa muda wote katika La Liga ikizingatiwa kwamba anajivunia jumla ya mabao 467 huku aliyekuwa fowadi matata wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo, akiwa na magoli 311 pekee. Ilivyo, huenda ikawa vigumu zaidi kwa rekodi ya Messi ya ufungaji wa mabao kambini mwa Barcelona na katika La Liga kuvunjwa na mchezaji mwingine yeyote.

Messi ambaye mkataba wake na Barcelona unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu, amefunga angalau mabao 20 ya La Liga katika kila mmojawapo wa misimu 13 iliyopita kwa mfululizo. Hiyo ni rekodi nyingine ya ufungaji wa magoli katika soka ya La Liga.

Chini ya kipindi cha miezi mitatu katika mwaka wa 2021, Messi tayari amepachika wavuni jumla ya mabao 15 kutokana na mechi 12.

Nyota huyo anayejivunia mabao 26 kutokana na michuano ya El Clasico, huenda akaongeza zaidi idadi hiyo ya magoli Barcelona watakapovaana na Real Madrid kwenye gozi jingine la El Clasico baada ya mechi za kimataifa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ole Kina na Buzeki kujiunga na ANC, adokeza Malala

Rais Samia Suluhu awapa Watanzania dira kuendelea kulenga...