• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Messi ampita Pele na kuweka rekodi mpya ya ufungaji mabao Amerika Kusini

Messi ampita Pele na kuweka rekodi mpya ya ufungaji mabao Amerika Kusini

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi amempita jagina Pele na kuwa mfungaji bora wa muda wote wa soka ya wanaume kwenye mechi za kimataifa miongoni mwa nchi za Amerika Kusini.

Hii ni baada ya mfumaji huyo mpya wa Paris Saint-Germain (PSG) kupachika wavuni jumla ya mabao matatu mnamo Alhamisi usiku na kusaidia timu ya taifa ya Argentina kupepeta Bolivia 3-0 katika mchuano wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Messi, 34, alikuwa mfungaji wa mabao yote matatu katika ushindi huo uliovunwa na Argentina jijini Buenos Aires. Nyota huyo wa zamani wa Barcelona sasa anajivunia mabao 79 kutokana na mechi 153 za kimataifa.

Nguli wa soka nchini Brazil, Pele, alikamilisha taaluma yake ya usakataji kabumbu akijivunia mabao 77 kutokana na mechi 92 za kimataifa.

Bao la kwanza la Messi dhidi ya Bolivia katika dakika ya 14 lilimwezesha kufikia Pele kabla ya kuvunja rekodi ya jagina huyo katika kipindi cha pili.

Baada ya mechi hiyo, Messi ambaye ni nahodha wa Argentina alijumuika na wanasoka wenzake kusherehekea taji la Copa America mbele ya mashabiki 20,000 wa nyumbani ugani Monumental.

Sogora huyo aliongoza Argentina kutwaa taji la kwanza la haiba kubwa katika soka ya kimataifa mnamo Julai 2021 baada ya kupepeta Brazil kwenye fainali ya Copa America jijini Rio de Janeiro.

“Nimekuwa nikitazamia sana siku hii na ninashukuru Mungu kwamba ndoto yangu imejibiwa,” Messi aliandika kwenye mtandao wake wa Instagram ambako pia alipakia picha za timu ya taifa ya Argentina na taji la Copa America.

“Sina maneno mwafaka zaidi ya kuwashukuru nyote – mashabiki na wachezaji wenzangu. Huu ni usiku ambao sitasahau kabisa katika maisha yangu. Ni tija na fahari tele kuwa nanyi katika safari hii,” akaongeza Messi.

Neymar Jr, 29, ambaye sasa anashirikiana na Messi katika safu ya mbele ya PSG, anajivunia mabao 69 kutokana na mechi 113 za kimataifa.

Kufikia sasa, Argentina waliotinga fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Brazil, wanashikilia nafasi ya pili nyuma ya Brazil kwenye orodha ya vikosi 10 vinavyowania tiketi nne za kunogesha fainali zijazo za Kombe la Dunia. Chini ya kocha Lionel Scaloni, Argentina wameshinda mechi tano na kutoka sare mara tatu katika jumla ya mechi nane zilizopita za kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Mwanasoka Marta ndiye anayeshikilia rekodi ya mchezaji aliyewahi kufunga idadi kubwa zaidi ya mabao miongoni mwa vikosi vya Amerika Kusini. Nyota huyo alifungia timu ya taifa ya wanawake nchini Brazil jumla ya mabao 109.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

MAPISHI: Weledi jikoni, vidokezo muhimu unavyopaswa kujua

Wabunge, maseneta wataka wanajeshi wapelekwe Laikipia...