• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 12:25 PM
MICHEZO: Kiota ambacho kinaelekea kufikia malengo ya kukomboa vijana na kuwa hifadhi la vijana wa kila jinsia.

MICHEZO: Kiota ambacho kinaelekea kufikia malengo ya kukomboa vijana na kuwa hifadhi la vijana wa kila jinsia.

Na PATRICK KILAVUKA

Mawazo pevu ya kuinua vipaji, kuangamiza visa vya utovu wa nidhamu na salama yalimpelekea kukumbatia vijana wa Landmawe, Nairobi West ambao walikuwa na talanta kujenga kiota cha timu ya Macmillan FC.

Muasisi Joseph Ochieng anasema akiwa bado mchezaji wa timu za Mathare United, Delaru na Kahawa Baracks, aliona vile vijana walikuwa wanateseka kupitia mawimbi ya vitendo viovu na moyo wa utu ukayagubia mawazo yake kuunda hifadhi hilo mwaka 2008.

Japo alianza na wavulana, jinsia imesawazika kwa kustawisha timu ya mabinti.Macmillan imefungamanishwa katika kategoria mbalimbali kuanzia U-9, U-12, U-13 na U-17 kisha ya wazima maskani yakiwa uga wa Landmawe.

Msimamizi muasisi Ochieng anakariri kwamba, ingawa halikuwa jambo rahisi mwanzoni kutokana na changamoto ya ukosefu wa ufadhili kwani alikuwa anagharamia mzigo wa timu pekee, anamshukuru Mola umbali timu imefika kwa sababu imetoa wachezaji ambao wanatambariza boli na kucheza ligi.

Imewahi kucheza Ligi ya Kanda ya Nairobi tangia kubuniwa kabla kushusha dimba katika kindumbwendumbwe cha Extreme Sports (SPS8) kuanzia 2012. Baadaye, ilirejelea Ligi ya Shirikisho la Soka Kenya, Kauntindogo, Nairobi West mwaka 2018 na kuibuka kidedee.

Picha/Patrick Kilavuka
Kikosi cha Macmillan FC kutoka Landmawe Nairobi West kikifanya mazoezi kabla kucheza dhidi FC Talents Ligi ya FKF, Kaunti,Nairobi West (NWCL) uwanjani Kihumbuni.

Aidha, msimu uliofuata, ilipandishwa ngazi ya Ligi Kaunti na kufikia msisitisho wa ligi kwa sababu ya msambao wa Corona, ilikuwa inashikilia nafasi ya nne mwaka jana.Msimu huu, wamecheza dhidi Shofco Mathare na kuwashinda 3-1, kufunga Potters FC 7-0, kuwachabanga Gachie Friends 2-0 Kabla kuwazima FC Talents 2-0.

Wadau ambao wamejitokeza kubadilisha maisha ya wanasoka hawa ni; kocha mkuu Peter Ambetsa, Kocha msaidizi Ramadhan Odhiambo na timu meneja Kelvin Baraza.Muasisi Ochieng anadokeza kwamba, si nia yao tu wachezaji wacheze soka mbali wapatie fursa ya kujitanua katika fani hii wakijifunza masuala mengine ya soka kama ukocha na urefa.

“Tunawaandaa wachezaji ambao watakuwa mduara kamili katika ulingo wa kandanda kwa kuwapa majukwaa ya kuendelea kujikuza kimaisha. isitoshe, twaazimia kuwahusisha katika kozi za masuala mengineyo pamoja na kuwapokeza ushauri kwa mujibu wa benchi.

Tayari kocha Ngige wa Muthurwa FC ni zao la mpango huo wa kuinua wachezaji ambao wamepitia timuni akiwa pia ni refa.Mbali na huyo, kunao wanakabumbu ambao wamefaulu katika nyanja ya soka ambao wanachezea timu zingine baada ya kushikwa mkono na Muasisi Ochieng kama mlinzi Dickens Mwema (Post Rangers), Westley Maziguru ambaye akiwa U-17 amezuru ughaibuini Norway, Italia na Korea Kusini, Samuel Mwangi (KCB) na Ezekiel Odera (City Stars).

Muasisi Ochieng alikariri kwamba, huu ni wakati wa makocha wa timu ya Primia wafaa kuchakuza vipaji vya soka mashinani kwani kuna wachezaji ambao wanaweza kucheza soka tamanifu kama njia kuinua vipaji vya kabumbu.Mipango ya timu ni kufika ligi za hadhi, kusaka wadhamini, kuwafanya wachezaji kufika viwango vya hadhi na kucheza hata ughaibuini.

Picha/Patrick Kilavuka
Kikosi cha Macmillan FC kutoka Landmawe, Nairobi West kikicheza dhidi FC Talents Ligi ya FKF, Kaunti,Nairobi West uwanjani Kihumbuni.
  • Tags

You can share this post!

Wanavoliboli wa Kenya ya ufukweni hawana corona, watawania...

Italia yapepeta Wales na kufikia rekodi ya kutoshindwa...