• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Nassir aongea kuhusu uhusiano wake na Ruto

Nassir aongea kuhusu uhusiano wake na Ruto

NA WINNIE ATIENO

GAVANA wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, ameelezea sababu za kuanza kushirikiana na Rais William Ruto, na viongozi waliochagulia kupitia mrengo wa Kenya Kwanza akisema ni kwa manufaa ya maendeleo.

Bw Nassir alisema bado yeye ni mwanachama wa ODM licha ya kushirikiana na Rais Ruto akisema hatua yake si ya kisiasa bali kwa maendeleo ya Kaunti ya Mombasa na kunufaisha wakazi.

Kwa kipindi cha mwezi mmoja, Bw Nassir amekuwa akishirikiana kwa karibu na viongozi wa serikalini huku Mbunge wa Nyali, Bw Mohammed Ali, na mwenzake wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya, wakimhimiza kuingia kwenye serikali.

“Rais alichaguliwa na Wakenya kama vile mimi. Ninatumikia Wakenya wote wale walionichagua, wale hawakunichagua na hata wale ambao hawakupiga kura. Ni vivyo hivyo lazima nifanye kazi na kila mtu. Viongozi wote wanashirikiana kwa manufaa ya wananchi,” akasema Bw Nassir.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Bw Nassir ambaye alikuwa mbunge wa Mvita kwa miaka 10 kabla awe gavana, alisema hajahama chama cha ODM.

“Nimekuwa ODM miaka yangu yote sijawahi kuhama vyama vya kisiasa. Pia, mimi ni Gavana wa Mombasa ni lazima nihudumie kila mtu bila ya kuangalia chama cha kisiasa. Heshima si utumwa, ninavyoheshimiwa na serikali ndivyo ninavyoregesha hisani hiyo,” akaongeza.

Alisema kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, ni mwanademokrasia na haoni ubaya akishirikiana na serikali ya kitaifa.
Bw Nassir alisema Wakenya wanafaa waelewe umuhimu wa watu kuishi kwa umoja, licha ya tofauti za kisiasa. Kulingana naye, ushirikiano wake na serikali ya kitaifa umemsaidia kuharakisha serikali ya kitaifa itoe leseni na vibali vitakavyowezesha wawekezaji kuwekeza kwenye eneo la viwanda maalum linaloanzishwa katika eneo la Miritini.

“Ingekuwa nina ugomvi au migogoro na serikali ya kitaifa hasa Rais Ruto, ningepata vibali hivyo?” akauliza.
Bw Nassir alisema lengo la viongozi wa Pwani ni kulinda maslahi ya wakazi wa eneo hilo na kuhakikisha wanapata maendeleo.
Mwanasiasa huyo alisema anafuata nyayo za marehemu babake, Shariff Nassir, ambaye alishirikiana na watu wa matabaka tofauti wakati alipokuwa kigogo wa siasa za Pwani.

“Tutapata nini tukiendelea kulumbana na serikali ya kitaifa? Sisi si maadui, lakini tumeimarika kisiasa. Lazima nifanye kazi na serikali ya kitaifa na wakazi wa Mombasa. Mvutano hautatusaidia,” akasisitiza.

Pia alipinga madai kuwa kucheleweshwa kutajwa kwa baraza lake imetokana na mvutano kati yake na wanasiasa wengine.

Alisema hivi karibuni atataja baraza lake kwani tayari alishachapisha nafasi za kazi hizo wazi.

“Hakuna mtu anaingilia uongozi wangu, hivi karibuni nitataja baraza langu. Kutakuwa na sura mpya ambayo itakuwa ya wataalamu. Lakini nani amesema hakuna wanasiasa wataalam?” akauliza baada ya kuulizwa endapo atateuwa wanasiasa kwenye baraza lake.

Bw Nassir na Mbunge wa Nyali waliamua kuweka kando tofauti za kisiasa ili kuleta maendeleo kwa wakazi wa kaunti hiyo. Bw Nassir alisema atashirikiana na wanasiasa wote ili kuhakikisha kaunti yake inanawiri, kwa kuwekeza katika miradi ya maendeleo.

Hivi majuzi, Bw Ali alisema Mombasa imepata mageuzi ya uongozi, akiapa kushirikiana na gavana huyo ili kuleta maendeleo.

Mbunge huyo wa Nyali kwa mara ya pili, alifichua kuwa, Bw Nassir amechukua jukumu la kuunganisha viongozi wote wa Mombasa.

Mbunge huyo na Gavana wa awali wa Mombasa Bw Hassan Joho, walikuwa na tofauti za kisiasa huku mbunge huyo akimlaumu, kwa kulinyima eneo bunge lake maendeleo.

Hata hivyo alisema ana matumaini kuwa uongozi ulioko, utaleta usawa na haki na kuimarisha sekta mbali mbali ikiwemo kuinua viwango vya elimu.

You can share this post!

Walimu wadai Sh1 bilioni wakijiandaa kupigania mkataba mpya

UTAFITI: Chuo chatafiti mitishamba kutathmini ufaafu wake

T L