• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Nimerejea Manchester United izaliwe upya – Ronaldo

Nimerejea Manchester United izaliwe upya – Ronaldo

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo amesema kwamba hajarejea Manchester United “kwa likizo” na kusisitiza kwamba ana hamu ya kuanza kuwajibikia mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) haraka iwezekanavyo.

Ronaldo ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, atatambulishwa rasmi kwa mashabiki wa Man-United kwa mara nyingine mnamo Septemba 11, 2021 uwanjani Old Trafford wakati wa mechi ya EPL Man-U itakapocheza dhidi ya Newcastle United.

Akisakatia Man-United katika awamu ya kwanza ugani Old Trafford, Ronaldo, 36, alifungia kikosi hicho jumla ya mabao 118 kutokana na mechi 292 katika kipindi cha miaka sita.

“Ningali na uwezo. Niko tayari kujituma ipasavyo,” Ronaldo alisema alipokuwa akitia saini mkataba wa miaka miwili aliyopokezwa rasmi na Man-United mnamo Alhamisi.

Kusajiliwa upya kwa Ronaldo kutoka Juventus kwa jumla ya Sh3.3 bilioni ni jambo lililogonga vichwa vya habari na kuzua gumzo kubwa katika ulingo wa soka ikizingatiwa kwamba sogora huyo wa zamani wa Real Madrid alikuwa akihusishwa pakubwa na Manchester City hadi siku alipohiari kurejea ugani Old Trafford.

Akiwa Man-United, nyota huyo ambaye ataendelea kuvalia jezi nambari saba mgongoni, alisaidia waajiri wake kunyanyua mataji matatu ya EPL, mawili ya League Cup, moja la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Kombe la FA.

Aidha, alisaidia kikosi hicho kutia kibindoni Kombe la Dunia kwa Klabu pamoja na taji la Community Shield chini ya kocha mstaafu Sir Alex Ferguson.

Ingawa Man-United wamejizolea mataji kadhaa tangu Ronaldo aagane nao na kuyoyomea Uhispania kuchezea Real mnamo 2009, kikosi hicho hakijawahi kutia kapuni ufalme wa EPL tangu 2012-13 kocha Ferguson alipostaafu.

“Hii ndiyo sababu niko hapa. Sijarejea Man-United kwa likizo. Nilijivunia misimu ya kuridhisha kambini mwa kikosi hiki miaka mingi iliyopita nikivalia jezi hii nambari saba. Sasa nalenga kushinda zaidi,” akasema Ronaldo.

“Ni fursa nzuri kwangu, kwa mashabiki na kikosi kizima kadri tunavyolenga kupiga hatua zaidi. Niko tayari na nadhani nitakuwa miongoni mwa wanasoka wanaostahiwa zaidi baada ya miaka mitatu au minne ijayo,” akaongeza.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

IPOA yaripoti ongezeko la idadi ya malamishi dhidi ya polisi

AKILIMALI: Ufugaji nyuki washika kasi biashara ya asali...