• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 7:55 PM
Nina kiu ya kunolewa na kocha Ronald Koeman – Memphis Depay

Nina kiu ya kunolewa na kocha Ronald Koeman – Memphis Depay

Na MASHIRIKA

MPANGO wa fowadi Memphis Depay kuingia katika sajili rasmi ya Barcelona umepigwa jeki na hatua ya sogora huyo raia wa Uholanzi kufichua kwamba ana kiu ya kutiwa makali na kocha Ronald Koeman.

Depay alitegemewa sana na Uholanzi katika ushindi wa 3-2 waliosajili dhidi ya Ukraine katika mechi ya Kundi C kwenye fainali za Euro mnamo Juni 13, 2021.

Nyota huyo kwa sasa hana klabu baada ya kuhiari kutorefusha muda wa kuhudumu kwake nchini Ufaransa mkataba wake na Olympique Lyon ulipotamatika rasmi mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

Depay, 27, aliwahi kunolewa na Koeman wakati ambapo kocha huyo alikuwa akidhibiti mikoba ya timu ya taifa ya Uholanzi almaarufu ‘The Oranje’.

“Mambo yatakuwa shwari na wazi zaidi baada ya mimi kupata mwajiri mpya. Kwa sasa ningependa kuachia mjadala huo hapo,” akatanguliza Depay.

“Kila mmoja anajua kwamba Barcelona wamekuwa wakiwania maarifa yangu kwa muda mrefu na ninahisi huu ndio wakati mwafaka zaidi wa kujiunga nao kwa sababu nimekuwa nikitamani sana kutia makali na Koeman,” akaongeza mwanasoka huyo huku akitaka mashabiki wake kuvuta subira zaidi.

Depay ambaye pia amewahi kuvalia jezi za PSV Eindhoven nchini Uholanzi, alifungia Lyon jumla ya mabao 76 kutokana na michuano 178 chini ya kipindi cha miaka mitano ya kuhudumu kwake katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

Mwanasoka huyo nusura asajiliwe na Barcelona mnamo Oktoba 2020 ila juhudi za kutua kwake ugani Camp Nou zikagonga mwamba.

Depay alikuwa na uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Uholanzi chini ya Koeman. Hata hivyo, uhakika huo ulishuka baada ya Koeman ambaye pia amewahi kuwanoa Southampton na Everton, kuyoyomea Uhispania kuwa mrithi wa Quique Setien ugani Camp Nou mnamo Agosti 2020.

Barcelona waliokamilisha kampeni za La Liga mnamo 2020-21 katika nafasi ya tatu jedwalini nyuma ya Real Madrid na viongozi Atletico Madrid, tayari wameanza kuisuka upya safu yao ya mbele kwa kujitwalia huduma za Sergio Aguero kwa mkataba wa miaka miwili.

Aguero ambaye ni raia wa Argentina, aliachiliwa rasmi na Manchester City kujiunga na Barcelona bila ada yoyote baada ya kandarasi yake ugani Etihad kutamatika mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Wanafunzi 94 kutoka Thika kupata ufadhili masomoni

Wakazi Naromoru wahimizwa kuzingatia sheria na mikakati ya...