• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 6:36 PM
TAHARIRI: Wadau wakuu sasa fanyeni jambo Stars irejee kileleni

TAHARIRI: Wadau wakuu sasa fanyeni jambo Stars irejee kileleni

NA MHARIRI

KIPUTE cha Kombe la Afrika (AFCON) kinapokamilika kesho kwa mchuano wa ndovu kumla mwanawe baina ya Senegal na Misri, inafedhehesha kuwa timu ya taifa ya kabumbu, Harambee Stars, haikufaulu kushiriki mwaka huu.

Tukitafakari ya nyuma kwa makini, iliichukua Kenya miaka 15 kabla ya kufuzu kwa dimba la AFCON mnamo 2019 nchini Misri.

Hata licha ya kufuzu kwa makala hayo yaliyopita, matokeo yake hayakuwa ya kuridhisha kwani Senegal na Algeria ziliirambisha Kenya sakafu kiaibu, kwa kuiadhibu Harambee Stars bila hata bao la kufutia machozi.

Kufuzu huko kuliwapa Wakenya hasa mashabiki wa soka matumaini ya kuifuatilia timu yao tena, ila hayakudumu kwani kama desturi, Kenya ilizua fedheha tena kwa kutunguliwa kidhaifu katika mechi za kufuzu kwa AFCON inayotamatika Cameroon kesho.

Vilevile, Stars ilidenguliwa majuzi katika kinyang’anyiro cha kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka huu nchini Qatar.

Swali ni je, Kenya ilikosea wapi? Katika historia ya kabumbu, Harambee imefuzu kwa kandanda ya bara mara sita tu.

Ila katika kufuzu huko, haikupita hatua ya makundi.

Mafanikio makubwa zaidi yanamweka kocha Mjerumani, marehemu Reinhardt Fabisch juu ya chati kama aliyewarejeshea Wakenya hamu katika kandanda baada ya kuiwezesha kuangusha timu kubwakubwa kama vile Algeria na Burkina Faso mbali na kutoka sare na majabali wa bara Nigeria.

Ni kutokana na ukufunzi wake wa hali ya juu mbali na utambuzi wa vipawa hasa kutoka maeneo ya mashinani (mashambani), si mijini tu, ambapo Fabisch alifanikiwa kuihuisha kandanda ya Kenya.

Naam, chini ya ukufunzi wake taifa hili halikufuzu kwa kipute hicho cha bara lakini inasadikika bila pingamizi kuwa ni kutokana na ‘mbegu’ aliyoipanda nchini ambapo Kenya hatimaye ilifuzu kwa makala ya mwaka 2004 yaliyofanyika nchini Tunisia.

Ikumbukwe kuwa ndiye aliyemtambua jagina wa soka nchini Dennis Oliech na wengi wengineo.

Aidha, inadhihirika kuwa kudumu kwa kocha kunamwezesha kuwaelewa wachezaji wake vizuri na hivyo basi kuzua uwezekano mkubwa wa timu kufaulu katika ishtighala zake za uchezaji.

Kwa hivyo, wadau katika sekta ya spoti na hasa mpira wa miguu, wanapaswa kufikiria mfumo wa kukuza mchezo kuanzia mashinani mathalani kwa kutambua vipawa kutoka pembe zote za nchi na kuanza kuvinoa hasa kupitia akademia za michezo jinsi inavyofanyika ughaibuni.

Kwa mantiki hiyo, tunayo imani kuwa mpya wa elimu (CBC) unaoshadidia ubainishaji na unoaji wa vipawa kuanzia utotoni, utarejesha taifa hili kileleni hasa katika fani ya kandanda. Tunatamani kuwaona kina Oliech wapya.

You can share this post!

VOLIBOLI: Kocha wa Prisons asema wako ngangari kukabili...

NYOTA WA WIKI: Sadio Mane

T L