• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 7:05 PM
Obiri, Mateiko waendea mamilioni ya Ras Al Khaimah Half Marathon

Obiri, Mateiko waendea mamilioni ya Ras Al Khaimah Half Marathon

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Hellen Obiri na Daniel Mateiko watatia kibindoni Sh14,325,603 kila mmoja ikiwa watashinda mbio za Ras Al Khaimah Half Marathon kwa rekodi ya dunia katika Milki za Kiarabu, Jumamosi.

Wawili hawa wanamezea mate mataji. Wanajivunia kasi bora kuliko wapinzani wao katika makala haya ya 16. Bingwa wa Afrika, Jumuiya ya Madola na dunia mita 5,000 na mbio za nyika Obiri anajivunia kukamilisha umbali huo wa kilomita 21 kwa saa 1:04:22.

Aliandikisha muda huo akikamata nafasi ya pili mjini Ras Al Khaimah mwaka mmoja uliopita, nyuma ya Muethiopia Girmawit Gebrzihair (1:04:14).

“Nafurahia kuanza mashindano yangu ya mwaka huu kwa kushiriki nusu-marathon hii ya haiba Jumamosi. Nimekuwa nikifanya mazoezi makali ili nitafute matokeo bora, na ikiwa hali ya anga itaniruhusu, natumai kuweka rekodi mpya ya Ras Al Khaimah na kurejea nyumbani kama bingwa,” Obiri alieleza tovuti ya mbio hizo.

Atapimwa vilivyo weledi wake na mshikilizi wa rekodi ya dunia mbio za kilomita 42 Brigid Kosgei pamoja na kundi la Waethiopia watano akiwemo Senbere Teferi. Wakenya Agnes Mumbua na Evaline Chirchir pia wako katika orodha ya wakimbiaji 14 watajika kinadada.

Tuzo ya kutwaa ushindi ni Sh1,713,501. Mtimkaji atatia mfukoni bonasi ya Sh12,611,417 akifuta rekodi ya dunia inayoshikiliwa na Mganda Jacob Kiplimo (dakika 57:31) na Muethiopia Letesenbet Gidey (saa 1:02:52).

Rekodi mpya ya Ras Al Khaimah Half Marathon itazawadiwa bonasi ya Sh685,403. Kiplimo na Gebrzihair wanashikilia rekodi za Ras Al Khaimah baada ya kushinda makala yaliyopita kwa dakika 57:56 na saa 1:04:14 mtawalia.

Mateiko alimaliza Ras Al Khaimah Half Marathon katika nafasi ya sita mwaka jana. Alipata muda wa dakika 58:26 alipomaliza Valencia Trinidad Alfonso nchini Uhispania katika nafasi ya tatu mwaka 2021.

Atapata ushindani mkali mkali kutoka kwa Wakenya Kennedy Kimutai (58:28), Felix Kipkoech (58:57), Weldon Langat (60:28), Richard Kimunyan (60:11) na Bernard Koech (59:57).

Bonasi ya kushinda taji la wanaume kwa chini ya dakika 58:15 na wanawake chini ya 64:30 ni Sh685,403.

Kuna zawadi pia kwa nambari mbili hadi tisa ambayo ni Sh1,199,457, Sh856,755, Sh616,863, Sh514,053, Sh342,702, Sh257,026, Sh188,486, Sh119,945 na Sh68,540 mtawalia.

Wakenya wa mwisho kutawala mjini Ras Al Khaimah ni Kibiwott Kandie na Fancy Chemutai mwaka 2020 na 2018 mtawalia.

  • Tags

You can share this post!

Mswisi na mpenziwe washtakiwa kwa kutolipa gesti Sh234,000

Trans Nzoia Falcons wanyorosha Kangemi Ladies kiboko kimoja...

T L