• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 1:16 PM
Trans Nzoia Falcons wanyorosha Kangemi Ladies kiboko kimoja cha uchungu katika KWPL

Trans Nzoia Falcons wanyorosha Kangemi Ladies kiboko kimoja cha uchungu katika KWPL

AREGE RUTH Na ORSBORN MANYENGO

BAO la mshambuliaji Lindah Nyongesa, lilitosha kuwapa Trans Nzoia Falcons alama tatu katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Kangemi Ladies katika mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL), ambayo ilichezwa ugani Ndura mjini Kitale leo Ijumaa.

Nyongesa ambaye alicheka na wavu dakika ya 11, ni bao lake la kwanza ambalo amefungia Falcons msimu huu.

Hata baada ya ushindi huo, Falcons wameendelea kusalia nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 10. Hizo ni alama sawa na za Zetech Sparks na Kisumu All Starlets ambao wanashikilia nafasi ya nane na tisa mtawalia.

Kangemi nao wako nafasi ya 11 na alama tatu. Wameshindwa kujikwamua kutoka kwenye hatari ya kushuka daraja baada ya mechi tisa za ligi. Wameshinda mechi moja na kupoteza mechi nane.

Mshambuliaji wa Falcons Joyce Makungu anaongoza kwenye orodha ya wafungaji bora kwenye timu hiyo na mabao matatu. Alifunga mabao matatu ‘Hattrick’ dhidi ya Kayole Ladies ambapo Falcons walipata ushindi wa 4-0.

Elizabeth Nafula ni wa pili na mabao mawili. Alifunga bao la kwanza dhidi ya mabingwa watetezi Thika Queens katika ushindi wa 2-0 katika mechi ya ufunguzi wa ligi na lingine dhidi ya Kayole.

Baada ya ushindi huo, mkufunzi wa Falcons Justine Okiring hakuficha furaha yake.

“Ingwa tumepata ushindi, mechi hiyo haikuwa rahisi. Tulitarajia tufunge mabao zaidi lakini Kangemi walikuwa wamejipanga vizuri zaidi kupambana na sisi,” alisema Okiring’.

Kwa upande wa Kangemi ambao wamefungwa jumla ya mabao 43 kufikia sasa, mechi dhidi ya Falcons ndio ya pekee ambayo wamefungwa bao moja pekee.

Kocha wa timu hiyo Collins Tiego alijitetea akisema, “Tulijipanga vizuri kucheza mechi hiyo lakini matokeo hayakuenda tulivyo tarajia. Waamuzi wa mechi pia wamakinike wanapochezesha mechi za wanawake. Kwenye mechi hii, kulikuwana upendeleo mkubwa upande wa wapinzani wetu.”

Mechi za ligi zinachukua mapumziko ya wiki moja. Ligi inatarajiwa kurejea tena Februari 25, 2023.

  • Tags

You can share this post!

Obiri, Mateiko waendea mamilioni ya Ras Al Khaimah Half...

Barcelona na Man-United nguvu sawa katika mkondo wa kwanza...

T L