• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 5:29 PM
Ongwae asalia nje Bungei aking’ara katika ushindi wa Bears dhidi ya Randers ligini Denmark

Ongwae asalia nje Bungei aking’ara katika ushindi wa Bears dhidi ya Randers ligini Denmark

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Tylor Ongwae Okari alisalia nje timu yake ya Bakken Bears ikilemea Randers Cimbria anayochezea Mkenya mwingine Preston Bungei 128-100 kwenye Ligi Kuu ya Mpira wa Vikapu Denmark mnamo Jumatano usiku.

Ongwae, ambaye ni mchezaji muhimu wa Bears, amekuwa mkekani tangu aumie mguu katika ushindi wa 119-92 dhidi ya Horsens IC mnamo Januari 31.

Alikosa ushindi wa Bears wa 96-76 dhidi ya Randers katika nusu-fainali ya Kombe la Denmark mnamo Februari 6, huku klabu hiyo ikithibitishia Taifa Leo siku mbili baadaye kuwa inatarajia arejelee mazoezi kati ya siku saba na siku 14.

Katika mahojiano na klabu hiyo siku ya Alhamisi, Bears ilisema kuwa Ongwae bado hajaanza kucheza.

“Tylor hafanyi mazoezi asilimia 100. Hata hivyo, ataruhusiwa kujiunga na timu ya taifa katika kipindi kijacho cha mechi za timu za taifa cha Shirikisho la Mpira wa Vikapu Duniani (FIBA) cha Februari 15-23. Atakuwa huru kuondoka baada ya mechi ya ligi inayokuja Jumamosi (dhidi ya Svendborg Rabbits),” aliongeza Mkurugenzi wa Michezo na Meneja Mkuu wa Bakken Bears, Michael Piloz.

Licha ya Randers kuzimwa, mzawa wa Amerika, Bungei aling’ara Jumatano. Alichangia alama 13, ‘rebounds’ 13 na pasi tano zilizozalisha alama.

Randers ilipoteza robo zote nne kwa alama 28-27, 34-21, 35-24 na 31-28. Itakutana na Horsens hapo Februari 13 kabla ya Bungei kuruhusiwa kujiunga na Kenya Morans inayofukuzia tiketi ya kuingi Kombe la Afrika (AfroBasket) ambalo haijafuzu kushiriki tangu iwe mwenyeji 1993.

Morans ni ya tatu katika Kundi B kwa alama nne. Iko nyuma ya viongozi Senegal (alama sita) na Angola (tano) nayo Msumbiji (tatu) inavuta mkia baada ya raundi ya kwanza iliyofanyika nchini Rwanda mwezi Novemba 2020.

Timu zitakazokamilisha kundi hili katika nafasi tatu za kwanza baada ya raundi ya pili na mwisho hapo Februari 19-21 jijini Yaounde, Cameroon zitafuzu kushiriki AfroBasket baadaye mwaka huu nchini Rwanda.

You can share this post!

Boateng kukosa fainali ya Kombe la Dunia kati ya Bayern...

Wanasoka 6 wa Ganze wafanyiwa majaribio na klabu za Mombasa