• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Patashika EPL Arsenal, Man-U wakisaka ubabe

Patashika EPL Arsenal, Man-U wakisaka ubabe

Na MASHIRIKA

ARSENAL watatua ugani Craven Cottage leo Jumapili wakilenga kukomoa Fulham na kuepuka presha kutoka kwa Manchester City – mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wanaokamata nafasi ya pili jedwalini.

Manchester United nao watapania kuweka kando maruerue ya kudhalilishwa na Liverpool 7-0 katika mechi iliyopita ya EPL kwa kuteremkia Southampton ugani Old Trafford.

West Ham United watakaribisha Aston Villa jijini London nao Wolverhampton Wanderers wapepetane na Newcastle United uwanjani St James’ Park.

Ushindi kwa Man-United utawadumisha katika nafasi ya tatu kwa alama 52 kadri wanavyofukuzia mataji matatu zaidi muhula huu baada ya kupiga Newcastle 2-0 ugani Wembley mwishoni mwa Februari na kuzoa ufalme wa Carabao Cup.

Kwa upande wao, Southampton wanakodolea macho hatari ya kuteremshwa ngazi msimu huu baada ya kuokota pointi 21 pekee kutokana na mechi 25.

Sawa na Fulham waliokubali kichapo cha 3-2 kutoka kwa Brentford katika pambano lao lililopita la EPL, Arsenal pia watakuwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kuambulia sare ya 2-2 dhidi ya Sporting Lisbon katika hatua ya 16-bora ya Europa League Alhamisi iliyopita nchini Ureno.

Kutandikwa huko kwa Fulham kulikomesha rekodi yao ya kutopigwa katika mechi saba mfululizo. Sasa wanajivunia alama 39 kutokana na mechi 26 huku pengo la pointi 24 likitamalaki kati yao na Arsenal wanaoselelea kileleni mwa jedwali.

Kuteleza tena kwa Fulham kutadidimiza zaidi matumaini yao ya kufuzu kwa soka ya bara Ulaya muhula ujao ikizingatiwa presha kali kutoka kwa Brighton, Brentford, Chelsea na Aston Villa ambao pia wamesakata idadi ndogo ya michuano.

Hata hivyo, Fulham wanajivunia kufunga bao katika kila mojawapo ya mechi sita zilizopita huku wakipoteza michuano mitatu pekee kati ya 13 iliyopita ambayo wamechezea katika uwanja wao wa nyumbani msimu huu.

Ingawa Fulham wamepoteza mechi 16 kati ya 18 zilizopita dhidi ya vikosi vinavyodhibiti kilele cha jedwali la EPL, waliwahi kuduwaza Chelsea mnamo Machi 2006 kabla ya kuangusha Man-United waliokuwa pia kileleni mwa jedwali mnamo Machi 2009.

Arsenal watajibwaga ulingoni wakiwa na rekodi nzuri ya kushinda mechi sita kati ya saba zilizopita katika EPL ugenini.

Aidha, wamefungwa mabao tisa pekee katika michuano yote ya hadi kufikia sasa ligini muhula huu na hawajawahi kupoteza dhidi ya Fulham tangu 2011-12.

Mchuano wa leo ni jukwaa maridhawa kwa kipa Bernd Leno na fowadi Willian Borges kupambana dhidi ya Arsenal ambao ni waajiri wao wa zamani.

  • Tags

You can share this post!

JUNGU KUU: Mipasuko yadhihirika katika Kenya Kwanza

PENZI LA KIJANJA: Urembo ni bonasi, gharimikia uhusiano

T L