• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:19 PM
Pique aagana rasmi na Barcelona na kustaafu soka

Pique aagana rasmi na Barcelona na kustaafu soka

Na MASHIRIKA

KIGOGO Gerard Pique, 35, aliagwa na mashabiki ugani Camp Nou kwa heshima na taadhima wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) iliyoshuhudia Barcelona ikitandika Almeria 2-0 Jumamosi usiku.

Beki huyo wa zamani wa Manchester United aliondolewa uwanjani katika dakika ya 84 na akapiga pambaja wachezaji wote wa Barcelona, kocha Xavi Hernandez na maafisa wote wa benchi ya kiufundi.

Pique atastaafu kwenye ulingo wa soka baada ya pambano la kesho litakalokutanisha Barcelona na Osasuna katika La Liga ugani El Sadar.

Akihojiwa mwishoni mwa mechi yao na Almeria, Pique alisema: “Nilizaliwa hapa na nitaaga dunia nikiwa hapa. Nina hakika kuwa nitarejea hapa Camp Nou baadaye maishani.”

“Ninapenda sana Barcelona. Japo naondoka, hii si kwaheri yangu ya mwisho. Nimebanduka tu kwa muda,” akaongezea.

Pique aliyevalia utepe wa unahodha dhidi ya Almeria, alizunguka uwanja mzima akiwa na wanawe wawili wa kiume. Wanasoka wengine katika kikosi cha Barcelona walivalia jezi zilizoandikwa jina la Pique na nambari tatu mgongoni.

Barcelona walipata penalti katika kipindi cha kwanza na mashabiki wakataka Pique aichanje. Hata hivyo, Mhispania huyo alimwachia mvamizi Robert Lewandowski aliyeipoteza.

Mabao ya Barcelona yalijazwa kimiani kupitia Ousmane Dembele na Frenkie de Jong. Miamba hao sasa wanajivunia alama 34 huku pengo la pointi 11 likiwatenganisha na Osasuna.

Pique anabanduka Camp Nou akijivunia kufungia Barcelona mabao 53 kutokana na mechi 616. Amenyanyulia kikosi hicho mataji 30 tangu ajiunge nacho kutoka Man-United mnamo 2008.

Alitangaza uamuzi wa kuangika daluga Alhamisi iliyopita licha ya kusalia na miezi 18 kwenye mkataba wake. Kuondoka kwake ni nafuu tele kwa Barcelona kifedha.

Zaidi ya kuwa na biashara nyingi, Pique anamiliki kikosi cha Andorra FC kinachoshiriki Ligi ya Daraja ya Pili nchini Uhispania. Ndiye mwanasoka wa tano kuwahi kuchezea Barcelona idadi kubwa zaidi ya mechi baada ya Lionel Messi (778), Xavi (767), kiungo wa sasa Sergio Busquets (694) na Andres Iniesta (674).

Ni Messi (35) na Iniesta (32) pekee ndio waliwahi kunyanyulia Barcelona mataji mengi zaidi kuliko Pique.

Pique alikuwa sehemu ya kikosi kilichozolea Uhispania ubingwa wa Kombe la Dunia na taji la Euro mnamo 2010 na 2012 mtawalia. Aliwajibikia kikosi hicho mara 102 kabla ya kuangika daluga kimataifa mnamo 2018. Ni mmoja kati ya wanasoka 13 wanaojivunia kuchezea Uhispania zaidi ya mara 100.

Alianza kutandaza soka kambini mwa Man-United waliomchezesha mara 23 kabla ya kumtuma Real Zaragoza kwa mkopo. Aliongoza Man-United kunyanyua mataji ya Community Shield, Ligi Kuu ya Uingereza na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2007-08.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Wenye rekodi mbovu kwa CRB kulipa riba zaidi

TALANTA: Kiongozi wa nyimbo

T L