• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 5:47 AM
Presnel Kimpembe aomba mashabiki msamaha baada ya kikosi chao cha PSG kuangushwa na Monaco ligini

Presnel Kimpembe aomba mashabiki msamaha baada ya kikosi chao cha PSG kuangushwa na Monaco ligini

Na MASHIRIKA

BEKI Presnel Kimpembe wa Paris Saint-Germain (PSG) alilazimika kuwaomba mashabiki wao msamaha baada ya kikosi chao kupokezwa kichapo cha 3-1 na AS Monaco katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) ugenini.

PSG waliokosa huduma za wanasoka Kylian Mbappe, Lionel Messi na Marco Verratti, sasa wamepoteza mechi mbili katika kipindi cha siku nne.

Wissam Ben Yedder aliandalia Aleksandr Golovin krosi safi iliyochangia bao la kwanza la Monaco kabla ya yeye mwenyewe kupachika wavuni magoli mawili.

PSG watakuwa wenyeji wa Bayern Munich katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Februari 14, 2023.

Mbappe ambaye ni mfungaji bora wa PSG msimu huu atakosa kuwa sehemu ya kikosi cha PSG kutokana na jeraha la paja. Ni matarajio ya kocha Christophe Galtier kwamba Messi atakuwa amepona jeraha la paja lililomweka nje ya pambano dhidi ya Monaco.

PSG walijikuta chini kwa mabao 2-0 baada ya dakika 18 za kipindi cha kwanza. Japo Warren Zaire-Emery aliwarejesha mchezoni, Ben Yedder alizamisha kabisa chombo chao kwa bao lake la 19 msimu huu.

Kimpembe alishushwa ngazi kutoka kuwa makamu wa nahodha wa PSG na nafasi hiyo kupokezwa Mbappe mwezi uliopita wa Januari 2023.

Licha ya kichapo, PSG ambao ni mabingwa watetezi wa Ligue 1 walisalia kileleni mwa jedwali la kipute hicho kwa alama 54, tano zaidi kuliko nambari mbili Olympique Marseille ambao pia wametandaza jumla ya mechi 23.

PSG sasa wamepoteza mechi tatu kati ya saba katika Ligue 1 mwaka huu wa 2023. Walichapwa na Monaco baada ya Marseille kuwadengua kwenye kivumbi cha French Cup mnamo Februari 8, 2023.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kiatu cha dhahabu KWPL chapata ushindani mkali

Timu ya taifa ya Ghana yapokeza Chris Hughton mikoba ya...

T L