• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 6:36 PM
PSG wafuatilia hali ya Ronaldo kambini mwa Juventus kwa nia ya kumsajili

PSG wafuatilia hali ya Ronaldo kambini mwa Juventus kwa nia ya kumsajili

Na MASHIRIKA

PARIS Saint-Germain (PSG) wanafuatilia hali ya Cristiano Ronaldo kambini mwa Juventus kwa lengo la kumsajili mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Hii ni baada ya rais wa zamani wa Juventus, Giovanni Gigli, kuwataka miamba hao wa soka ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kutemana rasmi na Ronaldo ambaye kwa mujibu wake, anachangia kuongezeka kwa gharama ya matumizi ya fedha kikosini humo.

Isitoshe, kocha Andrea Pirlo amenukuliwa na gazeti la The Sun akishauri kwamba fedha zitakazopatikana kutokana na kuuzwa kwa Ronaldo zitamwezesha kujinasia huduma za wachezaji chipukizi zaidi walio na uwezo wa kutambisha kikosi chake kwenye kampeni za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Licha ya kujivunia huduma za Ronaldo ambaye ni miongoni mwa wanasoka ghali zaidi duniani kwa sasa, Juventus waliaga mapema kampeni za UEFA msimu huu baada ya kudenguliwa na FC Porto kwenye hatua ya 16-bora mnamo Machi 9, 2021.

“Ni ghali sana kwa Juventus kuendelea kumdumisha Ronaldo kambini mwao. Niliwahi kusema hivyo aliposajiliwa kutoka Real, na bado nitasisitiza. Lengo la kuja kwake lilikuwa ni kusaidia kikosi kutwaa taji la UEFA, na sasa hali si hivyo,” akasema Gigli katika mahojiano na Radio Punto Nuovo nchini Italia.

Kwa mujibu wa Gigli, ambaye sasa amemtaka rais wa Juventus Andrea Agnelli kumwachilia Ronaldo ajiunge na PSG, mwanasoka huyo raia wa Ureno amekuwa akilipwa na Juventus kima cha Sh112 milioni kwa kila bao analowafungia.

Ronaldo ambaye pia amewahi kuchezea Sporting CP ya Ureno na Manchester United ya Uingereza, alisajiliwa na Juventus mnamo 2018 baada ya kushawishiwa kuagana na Real Madrid ya Uhispania kwa Sh9.8 bilioni.

Huu ukiwa msimu wake wa tatu kambini mwa Juventus, uwepo wa Ronaldo jijini Turin haujasaidia miamba hao wa soka ya Serie A kupiga hatua zaidi ya robo-fainali za UEFA.

Hata hivyo, kubwa zaidi ambalo Ronaldo amesaidia Juventus kufanya ni kuendelea kutwaa taji la Serie A kwa kipindi cha misimu miwili iliyopita. Kikosi hicho kwa sasa kinashikilia nafasi ya tatu jedwalini huku wakiwa nyuma ya AC Milan na Inter Milan wanaokamata nafasi mbili za kwanza kileleni.

Mkataba wa sasa kati ya Juventus na Ronaldo, 36, unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa Juni 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Roma, Villarreal na Ajax waweka hai matumaini ya kufuzu kwa...

Nabulindo aapishwa rasmi mbunge wa Matungu