• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 2:33 PM
Real watoka sare na Sevilla na kupoteza fursa ya kutua kileleni mwa jedwali la La Liga

Real watoka sare na Sevilla na kupoteza fursa ya kutua kileleni mwa jedwali la La Liga

Na MASHIRIKA

BAO la dakika ya mwisho kutoka kwa Diego Carlos aliyejifunga liliwavunia Real Madrid sare ya 2-2 katika gozi kali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Mei 9, 2021.

Matokeo hayo yaliwanyima Real ambao ni mabingwa watetezi wa taji la La Liga, fursa ya kupaa hadi kileleni mwa jedwali la kivumbi hicho.

Kombora la Toni Kroos katika dakika ya 94 lilimbabatiza Carlos na kuwezesha Real kusawazisha kwa mara ya pili na kupunguza pengo la alama kati yao na viongozi Atletico Madrid hadi pointi mbili pekee.

Fernandp Reges aliwaweka Sevilla kifua mbele katika dakika ya 22 baada ya kujaza kimiani krosi aliyopokezwa na Ivan Rakitic. Hata hivyo, Real walirejea mchezoni kupitia kwa Marco Asensio katika dakika ya 69 kabla ya Rakitic ambaye ni kiungo wa zamani wa Barcelona kufungia Sevilla penalti katika dakika ya 78.

Penalti ya Rakitic ilitokana na tukio la Eder Militao kuadhibiwa kwa kunawa mpira ndani ya kijisanduku dakika chache baada ya Karim Benzema naye kukabiliwa vibaya na kipa Yassine Bounou wa Sevilla.

Benzema alidhani alikuwa amewaweka Real uongozini baada ya kushirikiana na Alvaro Odriozola katika dakika ya 12 ila bao hilo likafutiliwa mbali na teknolojia ya VAR kwa madai kwamba Odriozola alikuwa ameotea.

Sasa ni alama mbili pekee zinazotenganisha vikosi vitatu vya kwanza kwenye msimamo wa jedwali la La Liga huku zikisalia mechi tatu pekee kwa kampeni za muhula huu kutamatika rasmi. Atletico wanaselelea uongozini kwa alama 77, mbili zaidi kuliko Real ambao wana idadi sawa ya pointi na nambari tatu Barcelona. Sevilla wanafunga orodha ya nne-bora kwa pointi 71.

Ushindi kwa Sevilla wanaotiwa makali na kocha Julen Lopetegui, ungaliwashuhudia wakipunguza pengo la alama kati yao na Atletico hadi pointi nne pekee. Awali, Atletico walikuwa wameambulia sare tasa dhidi ya Barcelona uwanjani Camp Nou.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Mamelodi Sundowns anayochezea beki Brian Mandela...

Rennes yadidimiza matumaini finyu ya PSG kuhifadhi taji la...